Kizimbani kwa kutaka kuiba mtoto albino

Muktasari:

Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wakikabiliwa na shtaka la kutaka kuiba mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ambaye ni albino kinyume na kifungu cha Sheria namba 169 (1) b sura ya 16 kanuni ya adhabu.

Vwawa.Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wakikabiliwa na shtaka la kutaka kuiba mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ambaye ni albino kinyume na kifungu cha Sheria namba 169 (1) b sura ya 16 kanuni ya adhabu.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Saada Salumu  alidai  washtakiwa walitenda kosa hilo Machi 16, mwaka huu saa 9.30 alasiri katika eneo la Nanyala, ambapo walijaribu kuiba mtoto huyo baada kufika nyumbani anakoishi na mzazi wake, Eda Nkota na kumchukua bila ridhaa ya mama yake.

Baada ya kumchukua mtoto huyo, msako mkali wa wananchi wa kijiji hicho ulifanyika na kisha kuwakamata washtakiwa hao kwa nyakati tofauti muda mfupi baadaye siku hiyo hiyo kabla hawajatokomea kusikojulikana.

Saada aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Tatizo Juma Mnozya (28) mkazi wa Kijiji cha Shitungulu na Robert Kamwela (29) mkazi wa Nanyala wilayani hapa. Hata hivyo, washtakiwa hao kwa pamoja walikana shtaka linalowakabili.

Mwendesha mashtaka huyo aliiambia mahakama kuwa katika shauri hilo atakuwa na mashahidi nane kutoka upande wa mashitaka.

Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Mbozi, Asha Waziri ambaye anasikiliza shauri hilo aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 26, mwaka huu itakapoanza kusikilizwa na kuwa dhamana kwa washtakiwa imezuiliwa hivyo wamerudishwa mahabusu.