Kodi ya VAT ilivyoumiza sekta ya utalii

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe

Muktasari:

  • Wadau, pia wamekasirishwa na uamuzi wa Serikali kupiga marufuku matumizi ya mkaa mijini, wakisema haijaweka mazingira ya kuwezesha uamuzi huo.
  • Suala la VAT katika huduma za utalii iliibua mjadala mkubwa mwaka jana, baada ya wabunge na waendeshaji huduma hiyo kupinga mpango huo kwa maelezo kuwa utawapa wapinzani wa Tanzania mwanya wa kuvutia watalii wengi.

Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akisoma hotuba yake ya bajeti leo, wadau wamerudia kilio chao dhidi ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma ya utalii.

Wadau, pia wamekasirishwa na uamuzi wa Serikali kupiga marufuku matumizi ya mkaa mijini, wakisema haijaweka mazingira ya kuwezesha uamuzi huo.

Suala la VAT katika huduma za utalii iliibua mjadala mkubwa mwaka jana, baada ya wabunge na waendeshaji huduma hiyo kupinga mpango huo kwa maelezo kuwa utawapa wapinzani wa Tanzania mwanya wa kuvutia watalii wengi.

Wakati Tanzania ikianzisha kodi hiyo, Kenya iliiondoa kwa lengo la kuvutia watalii waliopungua kutokana na matukio ya ugaidi.

Serikali ilisema ilitegemea kupata Sh7 bilioni kutokana na kodi ya VAT katika utalii, fedha ambazo zingesaidia kugharimia kutangaza utalii na pia kufidia upungufu wa mapato uliotokana na uwindaji kushuka.

Profesa Maghembe amesema wizara yake imejiwekea mkazo mkubwa kuhakikisha mchango wa utalii katika Pato la Taifa unafikia asilimia 20 kutoka asilimia 17.5 ya mwaka 2015/16.

Hata hivyo, wakizungumza na gazeti hili, wadau wa utalii waliohojiwa na Mwananchi walisema hali ya biashara ilikuwa ngumu kwa mwaka wa fedha unaoisha na kuna dalili kuwa hata msimu huu wa utalii hali ikaendelea kuwa mbaya.

“Hali bado ni tete,” amesema Daniel Mfugale, mkurugenzi wa Hoteli ya Peacock.

“Sisi kama watu wa hoteli tunafanya kazi na tour operators (waendeshaji huduma za utalii) ambao huwasiliana na watalii wanapokuja nchini. Watalii hufanya mipango ya safari mwaka mmoja kabla, sasa wanapoanza safari na kukuta ongezeko la kodi wanashindwa.”

Kauli ya Mfugale inalingana na ya Joel Marandu wa kampuni ya Mrere Company Ltd ambaye pia ni mwanachama wa chama cha Waendesha Huduma za Utalii (Tato).

“Kwa uzoefu wangu katika biashara ya utalii, kwa kweli watalii wamepungua sana mwaka huu,” amesema Marandu.