Koffi Olomide azuiwa kuingia Zambia

Mwanamuziki maarufu wa rhumba Koffi Olomide 

Muktasari:

Balozi wa Ufaransa nchini humo, Sylvain Berger, amesema atawashirikisha maofisa wa usalama wa Interpol kumkamata Olomide

Zambia. Mwanamuziki maarufu wa rhumba Koffi Olomide amezuiwa kuingia nchini Zambia kutokana na makosa mengi yanayomkabili katika taifa hilo.

Moja wapo ya makosa ni madai ya kumshambulia mpiga picha katika hafla moja ya muziki alipokuwa ziarani nchini humo.

Pia, anakabiliwa na madai ya kuwanyanyasa kingono wanenguaji wake, kuwateka nyara pamoja na kuwaajiri kwa njia ya udanganyifu.

Olomide,(62)  majina kamili Antoine Christophe Agbepa Mumba, alitarajiwa kuandaa burudani katika maonyesho mawili nchini Zambia mwezi huu, lakini serikali hiyo imemzuia.

Ubalozi wa Ufaransa nchini Zambia imejiunga na juhudi za kumkamata msanii huyo huku ikiitisha kukamatwa kwake siku ya Jumamosi wiki hii.

Balozi wa Ufaransa nchini humo, Sylvain Berger, amesema atawashirikisha maofisa wa usalama wa Interpol kumkamata Olomide, aliyesema kuwa bado mashtaka dhidi yake nchini Ufaransa hayajafutwa.