Komu na Kubenea kikaangoni Chadema

Muktasari:

  • Katika mkutano wa Kamati Kuu unaofanyika leo, Chadema pia inadaiwa kuwa huenda ikajadili suala la chaguzi ndogo zinazoendelea pamoja na wimbi la wabunge na madiwani wake waliohamia CCM

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema leo inakutaka kwa dharura kujadili masuala mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya chama hicho likiwamo la wabunge wake wawili, Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini).

Kubenea na Komu katika siku za hivi karibuni wamezua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa ni sauti yao inayosikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekana kuhusika na sauti hiyo kwa kile walichoeleza ni ya kutengeneza huku Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo (Chadema) naye akieleza kupeleka suala hilo ndani ya chama. Katika taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema, “Kikao hiki kitakuwa na ajenda kuu ya kujadili na kuazimia kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya chama.”

Taarifa hiyo ya Mrema ilisema, “Tutatoa taarifa rasmi juu ya maazimio ya kikao hiki kitakapomalizika.”

Licha ya Mrema kutobainisha iwapo suala la Kubenea na Komu aliyewahi kuwa mkurugenzi wa fedha wa chama hicho litajadiliwa kwenye kikao, Mwananchi limedokezwa na vyanzo vyake kuwa suala hilo linajadiliwa na wahusika wamealikwa.

“Ajenga kuu itakuwa ni hiyo ya hao (Kubenea na Komu) na ninafikiri wamekwisha kualikwa kuhudhuria kikao hicho, labda unaweza kufuatilia kwa kuwauliza wao kama wameshaalikwa,” kilieleza chanzo chetu.

Mwananchi lilipozungumza na Komu na Kubenea wote kwa nyakati tofauti walithibitisha kualikwa kwenye kikao hicho.

“Nimealikwa katika kikao hicho na nitakwenda kwa kuwa chama kimenialika,” alisema Kubenea.

Alipoulizwa uwepo wa taarifa kwamba chama kimepanga kuwatimua, mbunge huyo alisema, “Sijui walichokipanga, ila mimi nimealikwa na nitahudhuria.”

Kwa upande wa Jacob alisema kama chama kimeeleza kuwapo kwa kikao hicho na yeye atakuwapo.

“Mimi sina taarifa, lakini kama chama kimekuthibitishia kuwa kuna kikao, basi nimo kwa sababu mimi pia ni mjumbe wa kikao hicho,” alisema Jacob.

Katika ‘clip’ ya sauti iliyoanza kusambaa katika mitandao Oktoba 13 usiku, inasikika watu wawili wakizungumzia jinsi ya kumteka Jacob katika njia ya kumdhoofisha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Wanazungumza wakisema kama mpango huo utakamilika, basi Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itamuumiza kwani anampenda zaidi Jacob.

Pia, sauti hiyo inasikika wakisema suala la ruzuku za chama hicho zinaweza kumweka pabaya Mbowe kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) itafanya uchunguzi wa kina na hataweza kukwepa kutiwa nguvuni.

Mrema alipoulizwa jana kuhusu suala la Kubenea na Komu kama watajadiliwa alisema, “Kama tulivyosema, tutajadili masuala mbalimbali ya ndani na nje ya chama.”

Pamoja na masuala mengine, huenda kikao hicho kitakachokuwa chini ya Mwenyekiti Mbowe kitajadili ushiriki wa chama hicho kwenye uchaguzi mdogo wa majimbo ya Serengeti na Simanjiro ambako wabunge wake walijiuzulu na kujiunga na CCM.

Juzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza Desemba 2, kufanyika kwa uchaguzi huo pamoja na ule wa kata 21 za Bara. Wabunge waliojiuzulu kwenye majimbo hayo ni James Ole Millya (Simanjiro) na Marwa Chacha (Serengeti).

Wimbi la hamahama ya wabunge wake linaweza lisipite bila kujadiliwa kwani mpaka jana wabunge wake saba walikuwa wamejiuzulu na kujiunga na CCM kwa kile walichoeleza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli na wengine wakielekeza mashambulizi kwa Mbowe na chama hicho.