Korea Kaskazini yakataa kalamu ya Marekani

Muktasari:

Wakati ulimwengu ukifuatilia mkutano huo muda wa saa 2:00 hivi asubuhi kwa saa za New York, ofisa usalama katika msafara wa Kim alichukua na kuifuta mara kwa mara kwa kitambaa cheupe.

 


Washington, Marekani. Katika juhudi za kuhakikisha usalama wa Kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini Kim Jong un, ofisa wake wa usalama alifuta kwa kitambaa kalamu aina ya Sharpie iliyowekwa na Marekani kwa shughuli ya utiaji saini kabla ya dada yake kumpatia nyingine.

Kitendo hicho kilelenga kuhakikisha maofisa usalama wa Korea Kaskazini wanajilinda na kukwepa uwezekano wowote wa kiongozi wao kuwekewa sumu kwa namna mbalimbali.

Tukio hilo lilikuwa uthibitisho wa wazi namna Serikali ya Korea Kaskazini ilivyokuwa na hofu ya kuwekewa sumu, kwani msaidizi wake kwa umakini mkubwa alibadilisha kalamu kabla ya Kim Jong-un kuipokea kwa ajili ya kutia saini taarifa ya pamoja nchini Singapore.

Muda mfupi kabla Kim kuketi na Trump kumwaga wino kutia saini taarifa yao ya pamoja baada ya mkutano wao wa kwanza wa kihistoria kwa viongozi wa nchi hizo mbili, msaidizi wa kiume aliyevaa glovu nyeupe alichukua kalamu nyeusi iliyowekwa kwa matumizi ya Kim.

Wakati ulimwengu ukifuatilia mkutano huo muda wa saa 2:00 hivi asubuhi kwa saa za New York, ofisa usalama katika msafara wa Kim alichukua na kuifuta mara kwa mara kwa kitambaa cheupe.

Kisha, Kim na Trump waliingia ndani ya chumba kimoja, dada yake Kim, Kim Yo-jong alifuatia na akampita kaka yake na akampa kalamu tofauti aliyochukua kutoka mfuko wa jaketi lake. Picha za video zinaonyesha tukio hilo.

Kalamu hiyo mpya ndiyo alitumia Kim kusaini makubaliano yaliyoonyesha 'ahadi ya Korea Kaskazini' kufanya juhudi za kuelekea kuachana kabisa na silaha za nyuklia katika Rais ya Korea.”

Huo ulikuwa uthibitisho wa hivi karibuni wa tabia ya aina yake kutoka kwa kiongozi huyo wa utawala wa kurithi.