Korea Kusini kuimarisha umwagiliaji nchini

Muktasari:

  • Makubaliano hayo yatakayofanikishwa na Taasasi ya Korea Rural Community Corporation (KRC) yatagusia maeneo mbalimbali ikiwamo uimarishaji wa miundombinu hasa ujenzi wa mabwawa na mifereji ya umwagiliaji katika ukanda wa kusini, uliopo chini ya mpango wa Sagcot pamoja na kutoa elimu ya kilimo cha kisasa.

Dar es Salaam. Serikali ya Korea Kusini kwa kushirikiana na Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (Sagcot) wamesaini makubaliano ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuwasaidia wakulima hasa wa vijijini.

Makubaliano hayo yatakayofanikishwa na Taasasi ya Korea Rural Community Corporation (KRC) yatagusia maeneo mbalimbali ikiwamo uimarishaji wa miundombinu hasa ujenzi wa mabwawa na mifereji ya umwagiliaji katika ukanda wa kusini, uliopo chini ya mpango wa Sagcot pamoja na kutoa elimu ya kilimo cha kisasa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sagcot, Geoffrey Kirenga alisema wakulima wadogo watanufaika na kazi zao kutokana na mabadiliko yatakayoletwa na mpango huo.

“Kuna fursa nyingi lakini wakulima wengi wadogo wanakabiliwa na changamoto ya mtaji. Kilimo cha kisasa kinahitaji uwekezaji mkubwa na teknolojia ya hali ya juu, hivyo makubaliano haya yatatoa mwanga kwa wakulima wa vijijini,” alisema.

Balozi wa Korea Kusini nchini, Song Geum-young alisema urafiki wa Tanzania na Taifa lake umedumu kwa muda mrefu.

Rais wa KRC, Chung Seung alisema mpango walionao ni kuhakikisha wakulima wanakuwa na mifereji na mabwawa ya maji kwenye mshamba ili kuendesha kilimo cha mwaka mzima bila kutegemea msimu.

Alisema ujio wake umetokana na ombi la Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mathias Chikawe.

“Kutoka Japan hadi Korea Kusini ni mbali sana, nimezungumza na Balozi Chikawe kuhusu kusaidia maendeleo vijijini. Siwezi kumuangusha, kwa heshima yake nitahakiki-sha wakulima wadogo wananufaika,” alisema Seung.

Sagcot ni kituo kinachosimamia maendeleo katika sekta binafsi, tangu mwaka 2011 imekua mstari wa mbele kusaidia wakulima katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikishirikiana na Serikali na wadau wengine.