Korti yamzuia RPC kujibu swali la Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu

Muktasari:

Swali hilo lilimtaka RPC Hamdani kueleza anachokifahamu kuhusu Katiba ya Zanzibar na kama Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha anaweza kufuta matokeo ya uchaguzi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilimkataza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamdani kujibu swali la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye ni mshtakiwa katika kesi ya uchochezi.

Swali hilo lilimtaka RPC Hamdani kueleza anachokifahamu kuhusu Katiba ya Zanzibar na kama Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha anaweza kufuta matokeo ya uchaguzi.

Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema swali hilo halina msingi katika kesi hiyo na pia mahakama yake haina mamlaka ya kuzungumzia katiba ya visiwa hivyo, akisisitiza kuwa hata mwishoni mwa kesi hiyo hukumu haitaligusia.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Lissu, ambaye ni wakili wa kujitegemea na ameamua kujitetea katika kesi hiyo, alikubaliana na uamuzi huo na kesi itaendelea kusikilizwa Machi 8 na 9, 2017.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Simba baada ya Lissu, ambaye katika kesi hiyo ameshtakiwa pamoja na wahariri wa gazeti la Mawio, kumtaka Hamdani aeleze anachokifahamu kuhusu Katiba ya Zanzibar na kama Jecha anaweza kufuta matokeo ya uchaguzi.

Lakini wakili wa Serikali, Paul Kadushi alipinga shahidi huyo kujibu swali la Lissu, akidai kuwa RPC Hamdani si mtaalamu wa sheria wala katiba, hivyo hawezi kutoa tafsiri ya Katiba ya Zanzibar na pia mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza masuala ya kikatiba.

Lissu alidai kuwa pingamizi hilo halina msingi wowote kwa sababu suala la Serikali ya Zanzibar ni halali na limeletwa na upande wa mashtaka katika shtaka la pili na la tatu hivyo wakabiliane nalo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Ismail Mehboob, ambaye ni mchapishaji kutoka kampuni ya Jamana.

Wanakabiliwa na mashtaka matano, likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume cha Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002. Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao; Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho “Machafuko yaja Zanzibar”.

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, walichapisha habari hizo kwa lengo la kujenga chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Pia wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wasiweze kushiriki katika uchaguzi wa marudio wa Zanzibar.