VIDEO: Wabunge Kubenea, Komu wavuliwa uongozi Chadema

Muktasari:

Wabunge wa Chadema Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 wameomba radhi juu ya mazungumzo yao ya  mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob


Dar es Salaam. Wabunge wa chama kikuu cha Upinzani Tanzania Chadema, Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 wamevuliwa nafasi zao za uongozi.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika ametangaza uamuzi huo leo katika mkutano na waandishi wa habari ambao wabunge hao waliutumia kuomba radhi juu ya mpango wao hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob wakibainisha hawakuwa na nia ovu.

Mnyika alikuwa akisoma maazimio ya kikao cha kamati kuu kilichowahoji wabunge hao jana Jumatano Oktoba 17, 2018.

Amesema wabunge hao pia wamevulia uongozi ndani ya chama hicho huku wakiwekwa kwenye kipindi cha uangalizi wa miezi 12.

Kubenea na Komu katika siku za hivi karibuni wamezua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa kuwa ni sauti yao iliyokuwa ikisikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Jacob.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekana kuhusika na sauti hizo kwa kile walichoeleza ni za kutengeneza huku Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo (Chadema) naye akieleza kupeleka suala hilo ndani ya chama.

Lakini leo wamekiri kuwa sauti hizo ni zao na kuomba radhi wakibainisha kuwa hawakuwa na nia ovu.

Akisoma maazimio ya kamati kuu Mnyika amesema, “kamati kuu iliitishwa na ikafanya kikao chake juu ya tuhuma za utovu wa nidhamu wa wabunge hawa.”

“Baada ya kuhojiwa hatimaye kamati kuu ilifikia uamuzi  na kuwakuta na hatia ya ukiukwaji wa kanuni na maadili ya chama. Imewapa onyo kali kuwataka

waandike barua ya kuomba radhi kwa chama na kwa watajwa kufuatia maneno yaliyozungumzwa.”

Soma zaidi:

Akizungumza baada ya Mnyika kumaliza kusoma maazimio hayo, Kubenea amesema, “kama ambavyo mmelezwa nichukue nafasi hii kusema kwamba yaliyotokea siku hiyo ni bahati mbaya na hatukuwa na nia yoyote ovu kwa msingi huo naomba radhi wote walioguswa na watanzania kwa jumla.”

Kwa upande wake Komu amesema, “nichukue nafasi hii kwanza kwa kukishukuru chama kwa jinsi ilivyolichukulia jambo hili na kulipa uzito.”

“Chama ni kikubwa kuliko sisi wote na sisi ni vyombo vya chama, chama kina mikono yake. Kwa kutambua sisi ni vyombo vya chama tunatekeleza maagizo na tayari tumeshaandika barua za kuomba radhi.”

Komu amesema, “tunaomba radhi watanzania yale mazungumzo yetu yalikuwa ya faragha ila teknolojia ikatuzidi yakasambaa unajua mnavyokuwa kwenye faragha mnajiachia. Kwa hayo yaliyotokea tunaomba radhi, tunataka kuanza ukurasa mpya bila kuwa na kigugumizi.”