Kubenea, Nachuma wawa ‘mbogo’ tuhuma za kuhamia CCM

Muktasari:

Kubenea ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani ameeleza hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kukanusha tuhuma zilizokuwa zimeenea katika mitandao ya kijamii siku chache baada ya baadhi ya wabunge na madiwani kukihama chama hicho.

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema hakuna jambo lolote ndani ya chama chake litakalomfanya ang’atuke na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) hata kwa thamani ya fedha ya bajeti ya Taifa.

Kubenea ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani ameeleza hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kukanusha tuhuma zilizokuwa zimeenea katika mitandao ya kijamii siku chache baada ya baadhi ya wabunge na madiwani kukihama chama hicho.

Mbali na Kubenea, Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma ambaye naye alikuwa akihusishwa kukihama chama hicho na kujiunga na CCM, amewataka wananchi wa jimbo hilo kupuuza taarifa zinazosambaa kwamba ana mpango wa kujiondoa katika chama hicho.

Kuonyesha msisitizo, Kubenea aliwaambia wanahabari, “Siwezi kabisa kusaliti wananchi wa Ubungo, wananchi walionipigania. Kuna watu waliotoa michango yao ili niweze kuwa mbunge je, mimi ningewaangaliaje watu hao?”

Alisema kuna wajumbe wa kamati kuu ya Chadema ambao alishiriki kuwashawishi kujiunga na chama hicho hivyo isingeleta picha nzuri kwao kwa yeye kuhama.

“Mimi nitaendelea kuwa mbunge na makamu katika chama changu, nitakosoa na kushauri kama ilivyo kawaida yangu na bado ni mwanachama halali na sioni jipya upande wa pili kwani fursa ninazopata ni muhimu na kubwa,” alisema.

“Hizi zote ni njama za kutuvuruga lakini tupo imara na tutaendelea kutetea na kukosoa kila hali itakayojaribu kujitokeza.”

Nachuma

Akizungumzia madai ya kuhama CUF, Nachuma alikana na kusisitiza kwamba ataendelea kuwatetea wakazi hao ili wapate maendeleo.

“CUF hawana historia ya kuhamahama vyama, hata huyo aliyeondoka (Maulid Mtulia - Kinondoni), ameondoka kwa masilahi binafsi. Mimi Maftaha Nachuma nitakuwa wa mwisho kuondoka CUF,” alisema alipozungumza na mwandishi wetu jana.

Alisema suala la wabunge kujitoa katika nafasi zao linasababishwa na njaa na masilahi binafsi na si kutetea wananchi.

Nachuma alisema wabunge wengi walidhani wakipata nyadhifa hizo watakuwa wananufaika kwa kupata fedha, lakini hilo halipo kwa kuwa ubunge siyo dili, bali kuwatumikia wananchi.

Hakimu augua, dhamana wabunge wa Chadema yakwama Morogoro

Maombi ya dhamana ya wabunge wawili wa Chadema na washtakiwa wengine 37 yamekwama kusikilizwa jana baada ya kuelezwa kuwa hakimu anaumwa.

imeelezwa kuwa Hakimu Ivan Msack wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro anayesikiliza kesi hiyo ni mgonjwa hivyo kuahirishwa na washtakiwa kurudishwa rumande hadi kesho.

Akiahirisha kesi hiyo, Hakimu Erick Rwehumbiza alisema Msack amepata maradhi ghafla na alikuwa hospitalini kwa matibabu.

Baada ya maelezo hayo, upande wa utetezi ulimuomba Rwehumbiza kesi hiyo ihamishiwe kwa hakimu mwingine na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alisema kuahirishwa kwa kesi hiyo na kutotolewa dhamana kwa washtakiwa kunalenga kuchelewesha upatikanaji wa haki.

Kibatala pia ameiomba Mahakama iruhusu wananchi kuingia ndani ya ukumbi kufuatilia uendeshaji wa kesi hiyo.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Sunday Hyera alijibu hoja ya wananchi kuruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa Mahakama na kusema haina msingi katika kesi hiyo na hakuna uwezekano wa kuiwasilisha mahakamani.

Akijibu hoja hizo, Hakimu Rwehumbiza alisema alipewa jalada la kesi kwa ajili ya kuiahirisha tu na kuhusu dhamana, ombi hilo litashughulikiwa na hakimu anayehusika na iwapo hatakuwepo kesho wataangalia namna ya kuihamishia kwa hakimu mwingine.

Hakimu Rwehumbiza alisema suala la wananchi kuingia mahakamani haliathiri uendeshaji wa kesi na kwamba wanaweza kuwapo wawakilishi wao.

Wabunge Susan Kiwanga wa Mlimba na Peter Lijualikali wa Kilombero na washtakiwa wengine walifikishwa mahakamani Novemba 30 wakidaiwa kufanya uharibifu wa mali Novemba 26 katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi.

Wanadaiwa kuwa bila uhalali, huku wakijua wanatenda kosa, walikula njama na kuchoma moto ofisi ya kata na kufanya uharibifu wa mali.

Hakimu Msack alisema angetoa uamuzi wa dhamana juzi lakini hilo halikufanyika kutokana na kuibuka hoja za kisheria kuhusu hati ya kiapo ya kupinga dhamana iliyowasilishwa mahakamani hapo.

Kutokana na mvutano wa kisheria, hakimu Msack aliahirisha kesi hiyo hadi jana ili kutoa fursa kwa pande zote mbili kujibu hoja kuhusu hati hiyo.

Imeandikwa na Prosper Kaijage, Mary Sanyiwa na Hamida Shariff .