Wednesday, December 6, 2017

Kubenea asema hana mpango wa kuondoka Chadema

 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema hana sababu za msingi zinazomfanya kujiuzulu nafasi hiyo.

Pia, amewaonya wanaoeneza uzushi huo akitaka waache tabia hiyo.

Kubenea ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani amesema leo Jumatano Desemba 6,2017 saa saba mchana katika ofisi za kanda hiyo Magomeni Dar es Salaam, atakuwa na mkutano na waandishi wa habari.

Ametoa kauli hiyo baada ya taarifa kuenea kuwa ni miongoni mwa wabunge wa upinzani watakaohama vyama vyao katika dhana ya kuunga mkono utendaji wa Rais John Magufuli.

Akizungumza na MCL Digital, Kubenea amesema hajawahi kumweleza yeyote kwamba ana mpango wa kuhama na hafikirii kufanya hivyo.

“Sijawahi kukaa kuzungumza na CCM, hayo mambo ninayaona kwenye mitandao ya kijamii, kama kuna mtu ana ushahidi wa mimi kuzungumza na CCM autoe. Sina sababu za kuhama Chadema,” amesema Kubenea.  

Amesema, “Imani niliyopewa na wananchi wa Ubungo ni kubwa, siwezi kuichezea.”

-->