Kubenea kudai Tume huru ya uchaguzi bungeni

Mbunge wa jimbo la Ubungo (Chadema), Saed Kubenea akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Mbunge wa jimbo la Bukoba Mjini wa chama hicho, Wilfred Lwakatare. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Kubenea amesema amewasilisha barua ofisi ya Katibu wa Bunge mjini Dodoma.

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea amesema amepeleka bungeni barua ya kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ya kuwa na chombo huru cha kusimamia uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Machi 11,2018 Kubenea amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) si chombo huru cha kusimamia uchaguzi.

Amesema barua hiyo aliiwasilisha Alhamisi Machi 8,2018 katika ofisi ya Katibu wa Bunge mjini Dodoma.

Kubenea amesema uchaguzi kusimamiwa na Tume isiyo huru inaweza kusababisha machafuko.

"Hatuwezi kuacha hali hii iendelee, vurugu zimekuwa zikitokea kwa sababu ya kuwa na Tume ya aina hii, tunataka chombo huru," amesema.

Amesema tangu nchi iingie katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 uchaguzi umekuwa ukifanyika kwa kusimamiwa na Tume isiyo huru.