Kubenea kurudi mahakamani kupigania gazeti lake

Muktasari:

  • Mahakama hiyo Juni 21, 2018 ilitoa amri kwa Serikali kuhakikisha inachukua hatua stahiki ili gazeti hilo lirudi mtaani ikisema lilifungwa kinyume cha sheria.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kampuni ya Halihalisi inayochapisha magazeti ya Mawio, Mwanahalisi na Mseto, Saed Kubenea amesema watarudi Mahakama ya Afrika Mashariki kuomba kibali cha kuchapisha gazeti la Mseto baada ya Serikali kutoondoa zuio la uchapishaji.

Mahakama hiyo Juni 21, 2018 ilitoa amri kwa Serikali kuhakikisha inachukua hatua stahiki ili gazeti hilo lirudi mtaani ikisema lilifungwa kinyume cha sheria.

Gazeti hilo lilifungiwa Agosti 10, 2016 kwa miezi 36 ikielezwa ni kwa kuandika habari za upotoshaji, uchochezi na uongo, zisizozingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

 Kubenea akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Julai 22, 2018 amesema Serikali sasa inapaswa itoe ushirikianao kwa Mahakama ili usikilizaji wa kesi za madai na jinai ufanyike kwa haraka kuliko kucheleweshwa bila sababu za msingi.

"Tungekuwa tuna mitambo yetu tungekuwa tumechapisha tangu siku ambayo Mahakama imetengua agizo hilo lakini nashindwa kwa sababu wachapishaji wanahitaji hati ya usajili wa gazeti kabla ya kuchapishia,” amesema Kubenea.

“Lakini hicho kibali tutakachopewa na Mahakama kitatumika kama kigezo cha sisi kuchapisha na kuuza gazeti," ameongeza Kubenea ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema).

Wakili kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Fulgence Massawe amesema kitendo cha kuchelewa kutengua uamuzi wa kufungiwa kwa gazeti hilo ni ukiukaji wa sheria ambao unapaswa kuangaliwa.

"Siyo kwamba Serikali haina taarifa, siku hukumu inasomwa walikuwa na mawakili wa upande wa Serikali ambao walisikia na kuahidi kutekeleza maagizo," amesema Massawe na kuongeza:

“Serikali tayari imeandaa notisi ya rufaa kupinga hukumu hiyo na itaiwasilisha Jumatatu lakini jambo hilo halizuii kuanza kwa utekelezaji wa hukumu iliyotolewa,” amesema