Kubenea mikononi mwa polisi

Muktasari:

  • Mbunge huyo anashikiliwa polisi Oysterbay kwa ajili kusafirishwa Dodoma anakosubiriwa na Kamati ya Bunge

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea yupo mikononi mwa polisi akisubiri mchakato wa kusafirishwa kupelekwa mjini Dodoma kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi leo Jumanne, Kubenea amesema yupo katika kituo cha polisi cha Oysterbay  wilayani Kinondoni na akisubiri utaratibu wa safari ya kwenda Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa kama Spika wa Bunge Job Ndugai alivyoagiza.

Kubenea amesema awali kabla ya kushikiliwa alikwenda kujisalimisha polisi katika kituo hicho kisha aliambatana na askari hadi Katika Hospitali ya Aga Khan ambako alitakiwa kwenda kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha MRI.

“Baada ya kipimo kukamilika daktari alishauriwa nipumzike, lakini askari wakaamuru niondoke na kurudi Oysterbay. Hapa ninapozungumza na wewe nipo kituo nikisubiri kusafirishwa kwenda Dodoma,”amesema Kubenea na kuongeza kuwa;

“Hata hivyo, daktari ameshauri nisisafiri kwa njia ya barabara kutokana na matatizo ya mgogo niliyokuwa nayo hivyo nasubiri utaratibu hapa,” amesema mbunge huyo.

Akizungumzia kushirikiliwa kwa Kubenea, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema jeshi hilo lilikuwa na hati ya kukamatwa kupelekwa Dodoma kwa mbunge huyo ndiyo maana yupo mikononi mwao.

“Atapelekwa lini, atatoka saa ngapi au atasafirishwa kwa njia gani hilo mimi sijui ila atapelekwa Dodoma chini ulinzi wa polisi. Ukishakuwa na hati ya kukamatwa lazima utakaa mahabusu tu,”amesema Kamanda Mambosasa.

Hata hivyo, Kamanda Mambosasa amesema;“Kwanza sijui kama yupo polisi ndiyo kwanza nakisikia kwako,” alieleza.

Alipotafutwa mwenyekiti wa kamati hiyo, George Mkuchika kujua kama wajumbe wajumbe kamati yake, bado wapo Dodoma baada ya kikao cha Bunge kuhairishwa wiki iliyopita alijibu;

“Shughuli za kamati yangu hazifanyika katika magazeti, sisi tunafanya kimyakimya kisha  tunamkabidhi Spika wa Bunge,” alijibu Mkuchika kisha kukata simu.