Kukata mibuyu sasa kujaziwa fomu maalumu

Muktasari:

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Ahmad Kassim alitoa onyo hilo baada ya kuwapo taarifa za ukataji miti aina ya mibuyu katika kijiji cha Matemwe Mbuyupopo Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Zanzibar. Serikali imesema haitamvumilia mtu yeyote atakayekwenda kinyume na sheria katika mkatati wa miti ya asili ikiwamo mibuyu mikubwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Ahmad Kassim alitoa onyo hilo baada ya kuwapo taarifa za ukataji miti aina ya mibuyu katika kijiji cha Matemwe Mbuyupopo Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kassim alisema kutokana na ukataji miti ya asili kubwa kuwamo katika sheria, ni vyema ambao wanahitaji kukata wafuate taratibu ziliopo kinyume chake Serikali haitawavumilia kwa kufanya makosa kwa makusudi.

“Lazima ifahamike kuwa miti yote ya asili inapokuwa inahitaji kukatwa lazima mkataji azingatie taratibu na uhifadhi wa miti hiyo kwa mujibu wa sheria ziliopo, ikiwamo kujaza fomu maalumu ambayo itamwezesha kukubaliwa au kukataliwa ombi lake hilo,” alisema Kassim.

Alisema mkataji akiamua kwa makusudi kuikata miti hiyo bila kufuata taratibu zilizopo, Serikali ina uwezo kumchukulia hatua bila ya kujali sababu zozote.

Naye mkurugenzi wa idara ya misitu na maliasili zisizorejesheka Zanzibar, Sudi Juma aliwataka wananchi kuendelea kulinda mibuyu iliyoko katika vijiji vyao ili nchi izidi kuimarika kwa uhifadhi wa mazingira.

Akizungumzia suala hilo, sheha wa Matemwe, Vuai Farahani Mcha aliahidi kulinda maslahi ya kijiji chake sambamba na kusimamia sheria.