Kukutwa hai kwa mhandisi wa MV Nyerere kwawaibua wananchi

Muktasari:

  • Baada ya mhandisi wa Kivuko cha MV Nyerere kilichozama majini saa 48 zilizopita kuokolewa leo Jumamosi Septemba 22, 2018 akiwa hai, wananchi mbalimbali wamesema kama kazi ya uokoaji isingesitishwa juzi jioni Septemba 20, 2018  watu wengi zaidi wangeokolewa wakiwa hai

Ukerewe. Saa chache baada ya mhandisi wa Kivuko cha MV Nyerere kilichozama majini saa 48 zilizopita kuokolewa leo Jumamosi Septemba 22, 2018 akiwa hai, wananchi mbalimbali wamesema yaliyafika makosa kusitisha kazi ya uokoaji juzi jioni.

Wakizungumza na MCL Digital, baadhi ya wananchi hao walilaani kitendo hicho kwa maelezo kuwa huenda watu zaidi wangepatikana wakiwa hai.

Patrick Amos aliyempoteza mdogo wake katika ajali hiyo amesema kusitishwa kwa uokoaji kumechangia kuongezeka kwa idadi ya waliofariki dunia na kudai huenda walio hai bado wamo ndani ya kivuko hicho.

“Nashindwa kuelewa kabisa yaani chombo kimezama kikiwa na watu na ghafla mtu anasema uokoaji umesitishwa,” amesema Amos.

Janet Debora amesema, “Sidhani kama ni mimi tu ninayeshangazwa na jambo hili pengine ni dunia nzima. Kivuko kingekuwa hakionekani sawa, ila kipo juu kabisa na kinaonekana  na hata umbali kutoka nchi kavu ni kama mita 50 hivi.”

Sylvester Mkamwa mkazi wa Ukara amesema kusitishwa kwa uokoaji ni changamoto inayotokana na kikosi cha uokoaji kuchukua muda mrefu kufika eneo la tukio.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella leo ameieleza MCL Digital kuwa alisitisha kazi ya uokoaji baada ya kupewa ushauri wa wataalam wa uokoaji.

"Zoezi hili linafanyika kitaalam na wazamiaji wabobevu wanaofanya kazi kwa saa 24 ambao ilipofika usiku walishauri watu wasizame tena chini ya maji. Mimi kama msimamizi nisiye na utaalam wa kuzama majini sikuwa na namna nyingine zaidi ya kuwasikiliza," amesema Mongella

"Nisingetumia kofia yangu ya ukuu wa Mkoa na msimamizi wa zoezi la uokoaji kulazimisha waendelee kuzama kwa sababu uamuzi huo ungeweza kusababisha madhara zaidi ikiwemo kuwapoteza wataalam na kuongeza matatizo zaidi."