Kumbe marijuana ni imani?

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Leberatus Sabas akionyesha bangi iliyokamatwa

Muktasari:

Haya yanajitokeza wakati Serikali ikiimarisha mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya, watu wa imani ya Rastafari ambao hutumia bangi katika ibada zao kama sakramenti, wanasema aina hiyo ya kilevi si mihadarati.

Dar es Salaam. “Bangi ni sakramenti kwa Rastafari, kama divai katika makanisa ya Kikristo. Inatumika kiroho wakati wa kuomba, inatumika kwa kutafakari (meditation) wakati wa ibada,” anasema Mwenyekiti wa Umoja wa Marastafari Duniani, Thau-Thau Haramanuba aliyepo ziarani nchini.

Haya yanajitokeza wakati Serikali ikiimarisha mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya, watu wa imani ya Rastafari ambao hutumia bangi katika ibada zao kama sakramenti, wanasema aina hiyo ya kilevi si mihadarati.

Akijenga hoja kutetea matumizi ya bangi, Haramanuba alisema hata nchini Marekani kuna majimbo 26 yaliyopitisha kisheria bangi kama dawa huku nchi ya Afrika Kusini ikiwa mbioni kupitisha.

“Tunatumia nazi na mwanzi kama sehemu ya udongo, tunatumia moto kuchoma na maji kupoza.  Hiyo ni sehemu ya maombi kwenye ibada zetu. Unavuta unapitisha kwa mwenzako. Linaitwa bomba la amani, yaani unavuta huku ukitafakari.” Anasema.

Haramanuba anasema wamekuwa wakishauriana na Serikali ulimwenguni kutoingiza bangi kwenye dawa za kulevya ikiwa ni sehemu ya kudai haki zao. 

Jijini Dar es Salaam, moja ya mahekalu ambamo waumini wa Rastafari huvuta bangi wakati wote wa ibada zao kama sakramenti, lipo pembeni mwa Mto Ubungo ambao  unatenganisha eneo la Tanesco na Riverside.

Hekalu hilo liitwalo Melkizedeck House lililojengwa kwa nguzo za miti na kuezekwa mabati kama nyumba ya msonge, ni miongoni mwa mahekalu yaliyopewa majina mbalimbali kama Bob Ashant, 12 Tribes of Israel, Rastas na mengineyo na huongozwa na makuhani. Katika kila hekalu ibada zinapofanyika, bangi hutumiwa kama kichocheo.

Habari zaidi soma Mwananchi