Kuna ongezeko la biashara ya binadamu Afrika

Mkurugenzi wa idara ya ushirikiano wa kikanda, Balozi Innocent Shiyo 

Muktasari:

Biashara hii inatajwa kushika namba tatu katika orodha ya biashara haramu Afrika.


Dar es Salaam.Wakati hatua mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa ili kukomesha biashara haramu ya usafirishaji binadamu, kasi ya biashara hiyo imezidi kupaa na kuleta changamoto kwa nchi zilizo Kusini mwa Afrika.

Biashara hii inatajwa kushika namba tatu katika orodha ya biashara haramu zinazoingiza pesa nyingi nyuma ya biashara ya dawa za kulevya na uuzaji haramu wa silaha.

Hilo limewasukuma nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kukutana nchini Tanzania kujadili namna ya kukabiliana na tatizo hilo linalozidi kuota mizizi.

Akifungua mkutano wa siku nne uliozikutanisha nchi 16, mkurugenzi wa idara ya ushirikiano wa kikanda, Balozi Innocent Shiyo amesema umefika wakati nchi hizo kushirikiana kwa dhati kuikomesha biashara hiyo.

Amesema biashara hiyo inaonekana kuwaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake na watoto ambao wengi wao hurubuniwa kwa ahadi ya kutafutiwa kazi au kusomesha ughaibuni.

“Tatizo hili linazidi kukua na kushika kasi kwa kuwa inaonekana kuwa na pesa nyingi na watu wanazidi kujikita kwenye biashara hii, hivyo kupitia mkusanyiko huu kila nchi inakuja na changamoto inazokutana nazo na tutashirikishana namna ya kukabiliana nazo,”amesema Balozi Shiyo.

Kwa upande wake katibu wa sekretarieti ya kuzuia biashara haramu ya usafirishaji binadamu, Separatus Fella amesema tatizo la usafirishaji haramu wa binadamu litakwisha endapo kila mtu atashiriki kwenye vita hiyo.

Amesema hata hapa nchini bado jamii haijapata mwamko na wazazi wanaendelea kuruhusu watoto wao kutolewa vijijini kwa lengo la kutafutiwa kazi au kusomeshwa.