Kupatikana Mo Dewji gumzo vyombo vya habari duniani

Muktasari:

Vyombo mbalimbali vya habari duniani leo Jumamosi Oktoba 20, 2018 vimezungumzia tukio la kupatikana akiwa hai mfanyabiashara wa  Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo’ aliyetekwa Oktoba 11, 2018


Dar es Salaam. Ukiwa maarufu na kupatwa na jambo lolote lile ni wazi kuwa utatikisa kila kona. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.

Baada ya mfanyabiashara huyo kutekwa Oktoba 11, 2018 vyombo vya habari vya ndani na nje ya Tanzania vilizungumzia tukio hilo kwa kina kama ilivyokuwa leo Oktoba 20, 2018 mfanyabiashara huyo alipopatikana.

Gazeti la Daily Mail la nchini Uingereza ni miongoni mwa vyombo vya habari vilivyoripoti tukio hilo, likitumia habari iliyoandikwa katika mtandao wa gazeti la Mwananchi la Tanzania.

Daily Mail liliandika sehemu ya habari hiyo ya gazeti la Mwananchi iliyomnukuu Gullam Hussein, baba wa mfanyabiashara huyo akieleza kuwa mwanaye amepatikana akiwa salama.

Shirika la Utangazaji la CNN la nchini Marekani pia wamezungumzia tukio hilo, likinukuu kilichoandikwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba  ambaye alieleza kuwa mfanyabiashara huyo amepatikana.

“Mohammed Dewji amerudi nyumbani salama. Nimezungumza naye kwa simu dakika 20 zilizopita. Sauti yake inaonyesha yu mzima bukheri wa afya. Shukrani kwa wote kwa dua na sala. Naenda nyumbani kwake kumuona muda huu,” aliandika Makamba.

CNN wanasema walimtafuta baadaye Makamba na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya  Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kwa kupata habari zaidi lakini hawakupatikana.

Vyombo vingine vya habari vilivyozungumzia tukio hilo ni Shirika la Utangazaji la Ufaransa (RFI), Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Fox News, SKY News, AFP na  Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC).