Kupatikana kwa Mo Dewji kwazua mjadala mitandaoni

Muktasari:

Kupatikana kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ leo Oktoba 20, 2018 kumezua mijadala katika mitandao ya kijamii


Dar es Salaam. Kupatikana kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ leo Oktoba 20, 2018 kumezua mijadala katia mitandao ya kijamii.

Watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wanasiasa na wanaharakati wamehoji jinsi watekaji walivyomtupa Mo Dewji katika viwanja vya Gymkhana sambamba na gari wanalodaiwa kulitumia kukutwa  limetelekezwa karibu na uwanja huo.

Mo Dewji alitekwa alfajiri ya Oktoba 11, 2018 amepatikana leo saa nane usiku baada ya waliomteka kumtupa katika viwanja hivyo vilivyopo katikati ya Jiji  la Dar es Salaam.

Maria Sarungi amesema, “Watanzania mna maswali magumu sana! Ila sasa majibu sina hata mimi kuna mtu ananiuliza baada ya watekaji kumtelekeza @moodewji na gari pale Gymkhana karibu na Ikulu na ofisi nyeti za serikali na ubalozi, waliondokaje? Na @Uber ? Sina jibu mniacheee! #MoIsBack.”

“Kwa kifupi wamemrudisha Mo wenyewe! Tuliwaambia waliomteka #BringBackMo - basi wengine kelele nyingi eti kwa nini tunasema wamrudishe Sasa msituulize tena! Waliomteka walipata ujumbe na moto tuliutuma na maombi  wakamrudisha wenyewe. Tumefurahi sana umerudi mzima @moodewji.”

Msanii wa Bongo Fleva, Webiro N Wassira ameandika, “Aliyemteka Mo Dewji pengine anajiamini sana au sio mwenye akili timamu. Yaani anamteka mtu karibu na kwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na makao makuu ya usalama wa Taifa harafu anamtupa  karibu na Ikulu yaani bila uoga kabisa.”

Mchekeshaji Idris Sultan naye ameandika, “Tumejua marafiki zako na adui zako. Hakuna cha kutuzuia kwa sasa na sijui kama ni muda sahihi wa kuuliza ila Sirro ndo anapata ile hela eti? Au basi basi  pumzika kwanza.”

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara ameandika, “Naandika nafuta ,naandika nafuta, ahh!! Anaitwa Mungu Mwenye Enzi, Alhamdulillah!! Ngoja nitulize akili kwanza nitarufi baadaye.”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ameandika, “Nimemuona na kuongea kwa kirefu na Mohammed Dewji. Ni mzima wa afya isipokuwa ana alama za kufungwa kamba mikononi na miguuni. Mnamo saa nane usiku watekaji waliamua kumtupa kwenye maeneo ya viwanja vya Gymkhana. Naamini Polisi watatoa taarifa za ziada kuhusu kilichojiri.”

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema, “Ni Jambo la kumshukuru Allah leo @moodewji wamemrudisha akiwa salama mengine tutajadili wakati muafaka ila tunawashukuru kina Mkumbo ila kwa Nguvu ya Allah yatafika mwisho.”

Mbunge wa Arusha Mjini,  Godbless Lema amesema, “ “Namshukuru Mungu Mo Dewji amerudi salama. Nilikuwa niongee na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chadema leo saa tano. Nimeahirisha ili nione hii part 2 (sehemu ya pili) inaendeleaje, namwachia IGP Sirro amalizie sehemu hii kisha tutawataarifu ni wapi na lini tutakutana.”

Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe amesema “Namshukuru sana Mola ndugu yetu amerudi akiwa hai. Karibu sana @moodewji.”

Ismail Jussa amesema,“Kama kuna jambo moja kubwa la kujifunza katika sakata hili ni kwamba umoja ni nguvu.”