Kupotea kwa mwandishi wa Mwananchi Kibiti kwashtua wadau tasnia ya habari

Meneja Raslimali watu (HR) wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Aika Masawe (kushoto) akimsikiliza Anna Pinoni mke wa wa mwandishi wa kujitegemea wa MCL, Azory Gwanda aliyetoweka zaidi ya siku tisa, alipomtembelea nyumbani kwake Kibiti, mkoani Pwani jana. Kulia ni mtoto wa Azory, God. Picha na Beatrice Moses

Muktasari:

Taarifa ya mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Francis Nanai juzi ilieleza kuwa kutoweka kwake kuliripotiwa ofisini Novemba 30, ikiwa ni siku tisa baada ya kuagana na mkewe.

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeshtushwa na taarifa za kutoweka kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi mkoani Pwani, Azory Gwanda.

Taarifa ya mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Francis Nanai juzi ilieleza kuwa kutoweka kwake kuliripotiwa ofisini Novemba 30, ikiwa ni siku tisa baada ya kuagana na mkewe.

Kwa mujibu wa mkewe, Anna Pinoni (35), Novemba 21, asubuhi watu wanaokadiriwa kuwa wanne wakiwa na gari nyeupe aina ya Toyota Land Cruiser walifika sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara iliyo katikati ya mji wa Kibiti na kumchukua.

Katika taarifa hiyo inaeleza kuwa baada ya kumchukua, gari hilo lilielekea shambani kwake saa 4:00 asubuhi na kumkuta mkewe na Azory akaongea naye kuhusu safari ya ghafla kisha kuuliza ulipo ufunguo wa nyumba yao.

Taarifa ilisema Azory alimwambia mkewe kama asingerudi siku hiyo ya Novemba 21, angerudi siku inayofuata, lakini hajapatikana tena kuanzia siku hiyo.

Akizungumza na Mwananchi jana, katibu mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema wameshtushwa na taarifa hiyo.

“Huu ni ushahidi mwingine kuwa kazi ya uandishi wa habari ni ya hatari na mashaka. Si Azory pekee, kuna mwandishi mwingine wa Kasulu (Kigoma) na yeye alipotea na matukio mengine ya kutishwa na kuwekwa ndani kwa wanataaluma hii,” alisema Mukajanga.

Katibu huyo alisema ni wakati muafaka kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini kulinda usalama wa waandishi wao na mwaka kesho MCT itaweka programu ya mafunzo kwa wanahabari kufanya kazi kwenye mazingira hatarishi.

Mukajanga alivitaka vyombo vya dola kuendelea kumtafuta mwandishi huyo ili aweze kupatikana.

Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena aliungana na Mukajanga na kwa kuvitaka vyombo vya dola kumtafuta Azory kwa kuwa wameshapelekewa taarifa za kutoweka kwake.

“Uzuri wenyewe wanajua pa kuanzia ni wapi. Azory kabla ya kupotea alizungumza na mkewe, ni rahisi kwao,” alisema Meena.

Mtendaji huyo wa TEF alisema kupotea kwa mwandishi huyo kunaweka hofu kwa waandishi wengine na kwamba, wanaweza kushindwa kuandika habari za kuisadia jamii na badala yake wakakaa kimya.

Aliwataka waandishi wa habari kuchukua tahadhari, kama kutoa taarifa kwa viongozi wao wakati wa kutekeleza majukumu yao na wasikubali kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa zama zimebadilika.

Wakati huohuo, Chadema imesema imepokea kwa tahadhari taarifa za kupotea kwa mwandishi huyo na kulaani tukio hilo.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo habari na mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene imeeleza kuwa tukio hilo hadi sasa linadhaniwa kuwa na mazingira ya mwendelezo wa vitendo vya utekaji na mengine ya namna hiyo.

“Yalianza kujitokeza kwa wanasiasa, pia waandishi wa habari.Tunalitaka Jeshi la Polisi kumaliza utata wa kutoonekana kwa mwandishi huyu,” inaeleza taarifa hiyo. “Matukio haya yakiachwa bila kutafuta ufumbuzi wa haraka na kuyamaliza kabisa, tutakuwa tumeruhusu dalili mbaya kabisa za tishio la usalama wa raia mmoja mmoja na mali zao na hatimaye jamii nzima.”