Kutekwa kwa Mo Dewji, kampuni ya Mohammed Enterprises yakanusha kufunga shughuli zake

Muktasari:

  • Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Ltd (MeTL)  imesema inaendelea na uzalishaji na kukanusha taarifa ya kusitisha shughuli zake  kutokana na tukio la kutekwa kwa ofisa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’
  • Dewji alitekwa alfajiri ya Alhamisi ya Oktoba 11, 2018 katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kufanya mazoezi.



Dar es Salaam. Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Ltd (MeTL) imesema inaendelea na uzalishaji na kukanusha taarifa ya kusitisha shughuli zake  kutokana na tukio la kutekwa kwa ofisa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo. Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.

Kampuni hiyo imetoa taarifa hiyo leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 baada ya kusambaa kwa taarifa kuwa baada ya Mo Dewji kutekwa Alhamisi ya Oktoba 11, 2018, watasitisha huduma ifikapo Oktoba 20.

Leo kupitia ukurasa wa Twitter, uongozi wa kampuni hiyo umesema, “tunaendelea kusikitishwa  na tukio lililomtokea ofisa mtendaji wa kampuni yetu, Mohammed Dewji.”

“Pia, tunatoa ufafanuzi juu ya taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa Oktoba 20 tunasimamisha shughuli za uzalishaji katika kampuni yetu. Taarifa hiyo si ya kweli.”

Dewji alitekwa alfajiri ya Alhamisi ya Oktoba 11, 2018 katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kufanya mazoezi.

Juzi, familia ya mfanyabiashara huyo imetangaza donge nono la Sh1bilioni kwa atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa bilionea huyo kijana.