Kutimuliwa vigogo NSSF kwaibua mjadala

Muktasari:

MTAZAMO WA WASOMI

Akizungumzia uamuzi wa Bodi ya NSSF kuwaachisha kazi wafanyakazi hao bila kumgusa Dk Dau, mtafiti kutoka taasisi ya utafiti ya Repoa, Dk Abel Kinyondo alisema hilo linaibua maswali mengi.

“Ngumu sana kulielewa suala hili, kuna utata hapo kwa sababu kwanza, ni maswali baada ya mmoja kupangiwa kazi (Dk Dau) na wengine wasimamishwe, ilitakiwa wote wawekwe kundi moja...

Pili, sisemi kwamba haiwezekani kuwa msafi au siyo msafi ila unapotoa uchunguzi na kuwafukuza kadhaa huku mwingine anabakia salama, jamii haiwezi kuelewa. Sheria huwa inafuata fair treatment (utendaji usiopendelea).”

Mtazamo kama huo alikuwa nao Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangalla ambaye alisema uamuzi wa kumwacha Dk Dau ni ubaguzi na upendeleo wa wazi. “Kwanza kumteua balozi kabla ya matokeo ya uchunguzi ilikuwa tatizo, lakini hata matokeo yenyewe ya uchunguzi yasingeweza kumwacha salama. Wote walikuwa watuhumiwa sasa inakuwaje mmoja anateuliwa nafasi ya Serikali?” alisema.

Dar es Salaam. Baada ya Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwaachisha kazi maofisa wake waandamizi 12 waliokuwa wamesimamishwa tangu Juni mwaka jana ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikiwakabili, wadadisi wa mambo wameanza kuhoji kuhusu hatima ya aliyekuwa bosi wa taasisi hiyo, Dk Ramadhan Dau.

Pamoja na bodi hiyo kutangaza ajira mpya kujaza nafasi hizo, imesema bado inaendelea kufuatilia urejeshwaji wa fedha zote zilizopotea kwa njia ya ubadhirifu, ikizingatia taratibu stahiki na kusitisha miradi yote yenye mikataba mibovu.

Tangazo lililotolewa jana na NSSF, likiwa na orodha ya maofisa hao, limesema wameachishwa baada ya kubainika kuhusika katika ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na utaratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, ununuzi wa ardhi na ajira.

Walioachishwa kazi ni Yacob Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Mkurugenzi wa Fedha), Chiku Matessa (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala) na Sadi Shemliwa (Mkurugenzi wa Udhibiti, Hadhara na Majanga), Pauline Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani) na Crescentius Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji).

Wengine ni Amina Abdallah (Meneja Utawala), Abdallah Mseli (Meneja wa Uwekezaji), John Msemo (Meneja wa Miradi), Chedrick Komba (Meneja Kiongozi – Mkoa wa Temeke), John Ndazi (Meneja Miradi) na Ramadhani Nasibu (Meneja Mkuu Usalama).

Maofisa hao waandamizi walisimamishwa takriban miezi minne baada ya Dk Dau kuondolewa katika shirika hilo na kuteuliwa kuwa Balozi. Hivi sasa Dk Dau yupo Malaysia, kituo alichopangiwa Septemba mwaka jana na Rais John Magufuli.

Lakini jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe alimwambia mwandishi wetu kwamba Dk Dau hakuhusishwa katika uchunguzi huo.

Alisema wakati bodi hiyo inaingia madarakani, haikumkuta hivyo ililazimika kufanya uchunguzi kwa wafanyakazi wa shirika hilo pekee. “Yeye alikuwa tayari yuko nje kwa hiyo tusingeweza kumfuata huko,” alisema.

Alipoulizwa uamuzi wa kuwachunguza maofisa hao na kumuweka pembeni bosi wao, Profesa Wangwe alisema bodi hiyo iliamua mipaka iishie kwa wafanyakazi waliopo NSSF pekee. 

“Mipaka yetu iliamua iwe kwa waajiriwa wa NSSF, ndiyo maana hatukuhusisha hata wengine waliotakiwa kuchunguzwa kutoka nje ya NSSF,” alisisitiza.

Alipoulizwa ni kwa nini bodi haikumfuata Dk Dau huko Malaysia aliko, Profesa Wangwe alisema haitafuatilia mtu asiyehusika NSSF.

“Kuna vyombo vingine vinavyohusika vinaweza kufanya hiyo kazi ya kufuatilia zaidi,” alisema Profesa Wangwe akiwa mwenye haraka ya kuingia katika mkutano.

Tangu mwaka jana, gazeti hili lilichapisha mfululizo wa habari za uchunguzi zilieleza jinsi shirika hilo lilivyoingia katika kashfa ya mradi mkubwa wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni, Dar es Salaam wa Dege Eco Village ukidaiwa kugubikwa na ufisadi wa zaidi ya Sh179 bilioni.

Katika matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Bodi ya NSSF, imedaiwa kuwa watumishi hao kwa namna moja au nyingine au kwa uzembe uliopindukia au makusudi, wameliingizia shirika hasara, madeni na upotevu wa fedha.

“Kwa mfano, uchunguzi umebaini Sh12 bilioni zilikuwa zimetumika katika miradi ambayo haijaanza, matumizi ya Sh43 bilioni katika mradi ambao ulikwishaanza na baadaye kusitishwa, shirika kuingia mikataba mibovu inayowanufaisha wabia pamoja na kuwa na gharama kubwa isiyoendana na uwezo wa mtiririko wa fedha za shirika hivyo kusababisha ukwasi,” inaeleza taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo inadai kwamba watumishi hao wamelisababishia shirika kushindwa kukusanya zaidi ya Sh20 bilioni kutokana na utoaji wa mikopo isiyofuata utaratibu, shirika kufanya ununuzi wa viwanja bila kufuata taratibu huku baadhi vyenye thamani ya Sh18 bilioni vikiwa kwenye migogoro ya uvamizi.

Tuhuma nyingine dhidi ya maofisa hao ni kulifanya shirika kutekeleza miradi bila kufanya upembuzi yakinifu wa uhakika au kutofanya kabisa hatua iliyosababisha kutekeleza miradi ambayo gharama zake huongezeka zaidi ya mara tatu wakati wa utekelezaji na mwingine kuongeza gharama za miradi bila kupata idhini ya mamlaka husika.

Pamoja na hasara hizo, taarifa hiyo ya NSSF imewatoa hofu wanachama na wananchi kwa ujumla, “Bodi inauhakikishia umma kwamba, hali ya mfuko kwa sasa ipo salama kwa maana ya kutimiza majukumu kwa wanachama wote, mwenendo wa ukwasi umeimarika kutoka Sh12 bilioni ya Aprili 2016 hadi Sh354 bilioni kwa Juni mwaka huu. NSSF imelipa malimbikizo ya madeni mbalimbali, makusanyo ya michango yameongezeka kwa wastani wa Sh60 bilioni kwa mwezi kutoka Sh42 bilioni.”

Pia, taarifa hiyo inasema bodi kwa sasa inaendelea kusimamia nidhamu kwa watumishi, udhibiti wa matumizi mabaya ya fedha, kufuata kanuni, sheria na utaratibu katika uwekezaji na usimamizi wa miradi na ajira.