Kuunganisha umeme ni Sh 27, 000 tu

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza bungeni alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Wizara ya Nishati imeomba Sh1.7 trilioni kwa mwaka wa fedha 2018/19.



Dodoma. Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema gharama ya kuunganishia umeme ni Sh27, 000 na si vinginevyo.

Naibu Waziri huyo amesema hayo leo bungeni Mei 25, 2018 wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge walizozitoa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2018/19 ya Sh1.7 trilioni.

 “Uunganishwaji unaashiria rushwa na wizara yetu inakemea uwapo wa vishoka na gharama ni Sh27, 000 na wala haijabadilika,”amesema.

Mgalu ameagiza makandarasi na wasimamizi wa miradi ya umeme vijijini (Rea) kuwashirikisha viongozi wa maeneo wanaposambaza umeme ili kuainisha maeneno yenye kipaumbele.

Amesema wamepokea ushauri wote uliotolewa ikiwamo suala la baadhi ya vijiji na maeneo yenye taasisi nyeti kurukwa kutokana na kutokuwapo ushirikishwaji.

“Nitoe wito kwa wakandarasi na wasimamizi wetu saba wa kanda, kila mkoa na wilaya washirikishe viongozi wa serikali za mitaa, wabunge na wakuu wa wilaya ili kuanisha maeneno yenye kipaumbele,” amesema Mgalu.