Kuwait yafukuza wanadiplomasia wa Iran

Kuwait City, Kuwait. Mgogoro katika nchi za Ghuba umezidi kupanuka baada ya Kuwait kuamua kufunga Kituo cha Utamaduni cha Iran na ofisi nyingine na imewafukuza wanadiplomasia kadhaa, Shirika la Habari la KUNA limesema.

Mzozo huu unakuja wakati ambao Kuwait ni mpatanishi mkuu katika mgogoro unaohusu mataifa manne ya Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu dhidi ya Qatar inayodaiwa inafadhili ugaidi pamoja na vikundi vyenye itikadi kali kama Muslim Brotherhood.

Taarifa iliyotolewa na KUNA juzi inasema hatua hiyo ya Kuwait inahusiana na tukio la kuvunjwa ‘kigaidi’ gereza mwaka 2015 ambalo mamlaka zinasema lilikuwa na mkono wa Iran na Hezbollah. KUNA imesema Balozi wa Iran nchi Kuwait, Lireza Enayati amejulishwa kuhusu uamuzi huo.

Ofisa mmoja mwandamizi wa Kuwait, akizungumza kwa asharti la kutotajwa jina, aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kwamba wanadiplomasia 15 wamefukuzwa.

Alikataa kufafanua ikiwa Enayati alikuwa miongoni mwao lakini Shirika la Habari la Reuters limesema balozi huyo pia ametimuliwa.

Ofisa huyo pia alisema kwamba Kuwait imefunga ofisi zote za Iran zinazoshughulika na masuala ya “kijeshi, utamaduni na biashara”.

Kwa hasira, Iran imejibu ikidai kwamba madai ya wao kuwa nyuma ya kuvunjwa kigaidi kwa gereza moja hayana msingi wowote na italipiza kisasi.