Breaking News
Thursday, January 11, 2018

Kwa nini mawaziri hawamuelewi Rais-VIDEO

By Kelvin Matandiko Mwananchi kmatandiko@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli alipotangaza Baraza la Mawaziri la kwanza kwa Serikali yake, aliulizwa na waandishi wa habari kama atakuwa na semina elekezi kwa wasaidizi wake, jibu lake lilikuwa watajifunza wakiwa kazini.

Ilitarajiwa kuwa kwa kuwa alikuwa na utendaji tofauti na hakutaka kutumia fedha kuwaelewesha jinsi ya kuendana na kasi yake, angekuwa na uvumilivu kwa wale ambao hawakumuelewa vizuri.

Lakini miaka miwili tangu ateue timu yake ya kwanza, Rais Magufuli bado anawalalamikia baadhi ya mawaziri na watendaji wake kuwa hawamuelewi, hawaelewi Bunge linataka nini na wala mahitaji ya Watanzania licha ya kuwatumbua mawaziri na watendaji kadhaa tangu Mei 20 alipotengua uteuzi wa waziri wake wa kwanza, Charles Kitwanga.

Wakati fulani alifikia kusema baadhi ya mawaziri wake ni wapumbavu kwa kuwa wanashindwa kuchukua hatua, akitoa mfano wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iliyoshindwa kurejesha serikalini viwanda vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi.

Mara kwa mara Rais amesikika akilaumu jinsi watendaji wake wanavyoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, akitumia maneno kama “wakati waziri yupo, naibu waziri yupo, katibu mkuu yupo” lakini mambo hayajafanyika.

Mapema wiki hii alirudia tena kauli hiyo wakati wa hafla ya kumuapisha naibu waziri wa Wizara ya Madini, Dotto Biteko akisema uamuzi huo ameufanya ili “kuwaamsha waliolala” wizarani baada ya kushindwa kusaini kanuni za Sheria Namba 7 ya Madini iliyopitishwa Julai mwaka jana. Pia aliutaja udhaifu wa Wizara ya Kilimo kwa kushindwa kupeleka mbolea mikoani kwa wakati, ukiwemo Mkoa wa Rukwa ambao ni moja ya mikoa minne inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula.

Aliwahi kufanya hivyo kwa Wizara ya Fedha; Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kutoshughulikia magari yaliyohifadhiwa Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka miwili, yakiwemo magari ya Jeshi la Polisi.

Jumatatu alionekana kuwa mkali zaidi alipokuwa akizungumzia udhaifu wa kushindwa kusaini kanuni za Sheria ya Madini.

“Nasema hii kwa uchungu mkubwa kwa sababu baadhi ya ninaowateua bado hawajanielewa na inawezekana bado hawajaelewa Bunge linataka nini, Watanzania wanataka nini,” alisema Rais Magufuli.

“Na ndio maana nikaona labda ngoja niongeze naibu waziri aliyekuwa kwenye kamati ya madini, ili ushauri uliokuwa unatolewa na Bunge; ili haya mapendekezo yaliyopelekwa bungeni kupitia kamati yao, labda ataweza kutoa changamoto kwa watu waliolala, ambao bado wamelala ndani ya Serikali. Sifahamu Wizara ya Madini ina ugonjwa gani. Mtu unamteua pale, lakini sioni ile movement ninayoitaka and this is fact.”

Kauli hiyo ya Rais iliibua mjadala, hasa mitandaoni ambako kumekuwa kimbilio la wengi wenye madukuduku, baadhi wakilaumu wateule wake, wengine wakimlaumu Rais kwa maagizo tofauti na wengine wakisema kuna hofu inayosababisha baadhi wachelee kuchukua hatua.

“Kwa bahati mbaya, hajafanya replacement yoyote, lakini ni muhimu matamko anayotoa inabidi yaendane na mabadiliko ya kimfumo na mfumo ndiyo tunazungumzia taratibu za kisheria na miongozo ya utekelezaji wa maagizo anayotoa,” alisema Profesa Mohamed Bakari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Profesa Bakari alisema baadhi ya mawaziri wanataka kufuata utaratibu wa kawaida katika kufanya maamuzi yao, wakati Rais ana utaratibu mwingine.

Profesa Bakari alisema matamko ya kisiasa yamekuwa yakichukua nafasi kubwa kuhalalisha uchapakazi wa viongozi, bila kuangalia uhalali wa kisheria katika utekelezaji wa maagizo hayo licha ya kuwa na dhamira njema.

“Japokuwa yako maeneo mengine hayakuhitaji mabadiliko ya kimfumo na Rais ameingia tunaona mabadiliko. Kwa mfano, mfumo wa Jeshi la Polisi ni uleule na sheria, lakini kuna mambo yanabadilika, mfano katika eneo la rushwa. Kumbe changamoto ilikuwa ni usimamizi tu,” alisema.

Profesa huyo alisema sababu nyingine ni baadhi ya wateule kukosa uwezo wa kutafsiri maagizo yanayotoka juu.

“Wateule wanashindwa kutafsiri kwa uzito wake. Hili ni tatizo kubwa lililowahi kutokea mwaka 1971 baada ya Hayati Mwalimu (Julius) Nyerere kutoa miongozo baada ya Azimio la Arusha. Sasa Rais Magufuli ana vision yake,” alisema.

Alikuwa akizungumzia uanzishwaji wa vijiji ambao ulitekelezwa kwa mabavu na kusababisha baadhi ya watu kuumia wakati wa mchakato huo.

Alisema awali wakati mawaziri wakianza kutekeleza majukumu yao, kasi yao ilionekana lakini kwa sasa imepungua. Alisema kuna matamko yaliyohitaji kushughulikia kero za wananchi haraka, lakini yakakwamishwa na upatikanaji wa fedha. “Inawezekana wamegundua taratibu ni kikwazo, lakini tatizo jingine ni changamoto zilizopo nje ya uwezo wao,” alisema.

“Kwa mfano, unamuwajibisha mtendaji wa Tanesco kwa sababu ya mgawo wa umeme, kumbe ukichunguza unakuta tatizo liko nje ya uwezo wake. Upo umuhimu wa kuimarisha taasisi na kubadili miongozo ya kazi itakayoendana na kasi anayoitaka Rais.” Kwa upande wake, Profesa Benson Bana wa UDSM alisema mawaziri wanatakiwa kujifanyia tathmini ya utekelezaji wa majukumu yao. Alisema wapo baadhi wameonekana kupwaya katika kasi ya Rais Magufuli kutokana na kuathiriwa na mazoea ya utekelezaji wa majukumu wa miaka iliyopita.

 Profesa Bana alitilia shaka uwezo wa mawaziri hao katika utekelezaji wa majukumu waliyokabidhiwa.

“Rais anataka results (matokeo), hataki kusikia masuala ya mchakato sijui imefikia wapi, hataki utamaduni wa business as usual (mazoea),” alisema Profesa Bana.

“Wasipolifahamu hilo, wataumia mawaziri wengi sana. Kwa mfano unajiuliza kitu gani kilichelewesha kanuni baada ya sheria kusainiwa?”

Pengine kutomuelewa Rais kunaweza pia kukawa kunatokana na hatua tofauti anazochukua dhidi ya mawaziri. Wakati Kitwanga alibanwa na Bunge kutokana na kashfa ya Lugumi, Rais alimtengua kwa kosa jingine la kuingia bungeni akiwa amelewa.

Wakati aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye alipambana kutaka kushughulikia kitendo cha mkuu wa mkoa kuvamia kituo cha Clouds FM akiwa na askari wenye silaha, alijikutwa akiachwa katika Baraza la Mawaziri lililofanywa siku moja baada ya kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza suala hilo.

Wakati Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akionekana kufanikiwa katika vita dhidi ya ujangili, usafirishaji wanyamapori na ukataji misitu, alijikuta akiachwa katika mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa mwishoni mwa mwaka jana.

Wakati mawaziri waliosemwa hadharani kwa udhaifu hawajakumbana na uamuzi wa kutenguliwa kwa uteuzi wao, baadhi walichukuliwa hatua bila ya kusemwa awali hadharani.

Profesa Sospeter Muhongo hakuwahi kusemwa hadharani kwa kutochukua hatua baada ya Rais kutangaza kwa mara ya kwanza kuzuia usafirishaji mchanga wa madini nje. Alitenguliwa mara moja baada ya kutolewa kwa ripoti ya kamati aliyoiunda Rais kuchunguza suala hilo.

Rais alitangaza kupiga marufuku usafirishaji mchanga huo mwaka juzi, lakini haukuchukuliwa uamuzi wowote hadi alipoingilia kati suala hilo Machi, 2017.

Hii ni tofauti kwa mawaziri wengine. Dk Philip Mpango, ambaye ni Waziri wa Fedha, Charles Mwijage (Viwanda na Biashara), Profesa Makame Mbarawa (Uchuku), Dk Charles Tizeba (Kilimo na Chakula), Angela Kairuki (Madini) wamekumbana na maneno hayo makali ya Rais, lakini hawakutumbuliwa. Wakati mjadala kuhusu kauli ya Rais kuwa baadhi ya mawaziri wake hawamuelewi ukiendelea, swali la mwandishi aliyetaka kujua kama kutakuwa na semina elekezi kwa wasaidizi hao, linaweza kuwa na mantiki sasa.

-->