LHRC: Watoto 2571 wamebakwa

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Dk Hellen Kijo-Bisimba.

Muktasari:

Takwimu hizo zilitolewa jana wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya kituo hicho tangu kuanzishwa kwake.

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema takwimu zinaonyesha kwamba kati ya Januari na Julai mwaka huu, watoto wa kike na kiume 2,571 walibakwa na kulawitiwa hapa nchini.

Takwimu hizo zilitolewa jana wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya kituo hicho tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema takwimu hizo zinaweza kuongezeka kutokana na watu wengi kutotoa taarifa za ubakaji na ulawiti Polisi.

Alisema takwimu hizo ambazo zimetoka katika Jeshi la Polisi zinaonyesha kwamba kati ya matukio hayo, kesi 1,203 bado ziko katika hatua ya upelelezi wakati kesi 822 zipo mahakamani na watuhumiwa 234 walishahukumiwa.

Akifafanua zaidi, alisema takwimu hizo zinaonyesha  kwamba katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, kulikuwa na matukio kama hayo 1,765.

“Matukio haya yanazidi kuongezeka kwa sababu mwaka 2015 katika kipindi cha Januari hadi Machi kulikuwa na matukio   1,585 ya watoto kubakwa na kulawitiwa,” alisema.

Bisimba alisema jambo la kusikitisha ni kwamba wahusika wakuu wa matukio hayo ya ubakaji na ulawiti ni wanafamilia wa karibu wa watoto hao.

“Wazazi na walezi tunatakiwa kuwa makini na watoto wetu,” alisema Bisimba kabla ya kutoa misaada mbalimbali ya vyakula na nguo kwenye Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini wilayani Temeke.

Wafanyakazi wa LHRC walitumia siku nzima ya jana kucheza na watoto hao ili kuwapa faraja.

Kwa taarifa hii zaidi na nyingine nyingi  nunua gazeti lako la Mwananchi kesho au soma mtandaoni BONYEZA HAPA