LHRC yampongeza Rais Magufuli kutotekeleza adhabu ya kifo

Mwanasheria ambaye pia ni Mkurugenzi wa utetezi na maboresho, Flugence Massawe akizungumza na vyombo vya habari leo, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Felista Mauya. Picha na Herieth Makwetta

Muktasari:

Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) kimesema licha ya Rais Magufuli kusema hatatekeleza hukumu ya kifo katika kipindi chake, Oktoba 9, 2018 kimefungua kesi ya kikatiba namba 22 ya mwaka 2018 kupinga uwepo wa adhabu ya lazima ya kifo.


Dar es Salaam. Wakati watu 472 nchini Tanzania wakiwa wamehukumiwa adhabu ya kifo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kinatambua mchango wa Rais John Magufuli katika kutetea haki za binadamu.

Akizungumza leo Oktoba 10, 2018 katika maadhimisho ya 16 ya siku ya kupinga adhabu ya kifo duniani, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Felista Mauya amesema kituo hicho kinatambua mchango wa Rais wa Awamu ya Tano.

“Tunampongeza Rais John Magufuli, alisema hadharani kwamba hatatekeleza hukumu ya kifo katika kipindi chake na kutoa msamaha kwa wafungwa 62 waliohukumiwa kunyongwa tukio ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Tanzania,” amesema Mauya.

Katika hatua nyingine Mauya amesema Tanzania kwa sasa ipo katika hatua isiyo rasmi ya kupinga na kutotekeleza adhabu ya kifo japo hakuna jitihada za lazima zilizochukuliwa kuonyesha nia ya kuifanya hali hiyo kutambulika kisheria.

“Kama sehemu ya maadhimisho Oktoba 9, mwaka huu kituo kimefungua kesi ya kikatiba namba 22 ya mwaka 2018 kupinga uwepo wa adhabu ya lazima ya kifo kwa kuzingatia mifano ya nchi jirani kama Kenya, Uganda na Malawi ambapo adhabu ya lazima ya kifo imefutwa kabisa,” amesema.

Mwanasheria ambaye pia ni Mkurugenzi wa utetezi na maboresho, Flugence Massawe amesema sheria hizo zinatakiwa zirekebishwe ili zitoe nafasi zaidi kwa mahakama na wale wanaoshtakiwa.