LHRC yatimiza miaka 23 tangu kuanzishwa

Muktasari:

  • Leo Septemba 26, 2018 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimetimiza miaka 23 tangu kianzishwe huku kikijipatia mafanikio sambamba na changamoto ikiwamo kuhusishwa na siasa

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) leo Jumatano Septemba 26, 2018 kimetimiza miaka 23 tangu kuanzishwa kwake huku kikijivunia kuwajengea uwezo Watanzania juu ya sheria na haki za binadamu.

Akizungumza leo mkurugenzi mtendaji  wa LHRC, Anna Henga amesema katika miaka 23 ya utendaji kazi wa kituo hicho kumekuwepo na uelewa mkubwa wa haki na sheria nchini.

Amesema kituo hicho kimekuwa chachu ya mabadiliko ya sera na kutungwa kwa sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya msaada wa kisheria ya mwaka 2017.

Henga amesema LHRC imeibua mambo mbalimbali yaliyopelekea uwajibikaji katika ulinzi wa rasilimali za nchi.

Sanjari na mafanikio hayo Henga amesema kituo kimekuwa na changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na kuhusishwa na shughuli za kisiasa.

"Sisi si wanasiasa ila tunaweza kumtetea mwanasiasa endapo haki zake zitakiukwa hivyo si sahihi kutuhusisha na shughuli za kisiasa," amesema.

"Hii hupelekea wananchi kuamini propaganda zenye lengo la kudhoofisha juhudi za kituo za kuifikia Tanzania inayoheshimu misingi ya haki za binadamu na utawala bora."