MAKALA: Lowassa ni rafiki yetu, ndugu yetu na jamaa yetu wa karibu

Muktasari:

Awe Ikulu au mitaani tutaendelea kumpenda.

Bado Edward Lowassa yuko kwenye vinywa vya wananchi. Wanamjadili hasa baada ya ziara yake ya ikulu na kauli zake zilizofuata, licha ya kuwa huu si wakati wa kampeni za urais.

Lowassa ni rafiki yetu, ndugu yetu, jamaa yetu wa karibu na pengine tunasali kanisa moja na kushiriki pamoja jumuiya. Huyu ni mtu tunayemfahamu vizuri. Tunampenda na hakuna wa kututenganisha naye, tulimpenda jana, tunampenda leo na tutampenda hata kesho.

Awe Ikulu au mitaani tutaendelea kumpenda. Urafiki wetu ni wa kudumu na wala si urafiki wa barabarani. Kama yeye alivyosema huko nyuma kwamba yeye na Rais Jakaya Kikwete, hawakukutana barabarani, na sisi pia uhusiano wetu si wa barabarani.

Lowassa ni mtu mwema, anawapenda sana watu. Ana marafiki wengi na wa miaka mingi. Huwezi kumpata kiongozi hapa Tanzania, mwenye marafiki wengi kama Mheshimiwa Lowassa. Huyu hana tabia ya kuwasahau ndugu na rafiki. Anapenda kukutana na marafiki, kula nao na kunywa nao. Ni mtu anayependa sherehe na kufurahia na ndugu na marafiki. Ni mtu wa msaada, ukimwendea na shida, ni lazima atakusaidia. Kwenye nafasi zote alizoshika, kuanzia uwaziri, hadi uwaziri mkuu, alihakikisha amewasaidia rafiki zake na watoto wa rafiki zake. Wote walipata kazi.

Lowassa, ni mcha Mungu, anapenda kusali na analipenda kanisa lake na viongozi wake. Yuko mstari wa mbele kusaidia makanisa hata na misikiti. Ana marafiki wengi viongozi wa dini mbalimbali. Akiingia kanisani ni lazima atoe sadaka nzito. Viongozi wengi wa dini wamempenda sana kwa moyo wake huo wa kupenda kusaidia.

Wanaosema anapenda madaraka wanamsingizia. Yeye anapenda kuwatumikia watu, anapenda kuzungukwa na watu na kusikilizwa na watu. Ana tabia kama ya machifu wa zamani. Tena badala ya kusema anapenda madaraka au ana uchu wa madaraka, ni bora waseme huyu ni chifu. Alikuwa hivyo, maisha yake yote, waliosoma naye, wanamkumbuka kwa tabia hiyo ya kutaka kuzungukwa na watu na kuonekana kwamba yeye ndiye kiongozi wao, au yeye ndiye anayewaunganisha. Kwa tabia hiyo, alijenga mtandao ndani ya CCM, na mtandao huo unaendelea hadi leo hii. Hatupendi kuingia kwa undani juu ya mtandao, lakini sote tunafahamu kwamba mtandao huu ulikuwa na faida chanya na hasi. Na kwa wastani, hasi ni kubwa kuliko chanya. Mtandao huu umejenga makundi ndani ya CCM na kuivuruga. Mtu, anayejenga makundi kwenye jamii hawezi kuwa kiongozi bora zaidi ya kuwa mfalme. Sote tunakumbuka kwamba wafalme walikuwa watawala na wala hawakuwa viongozi. Dunia ya leo inatafuta viongozi na wala si watawala.

Lowassa, ni mtu wa watu, ni mtu mwema, mtu mwenye kuwajali watu. Nikisema huyu hawezi kuwa Rais mzuri, si kwamba ninamchukia hapana. Ninasema hivyo kwa sababu ninamfahamu. Ninajua kabisa kwamba “tabia ya uchifu” haiwezi kuruhusu awe rais mzuri. Atakuwa mtawala, na sisi muda wote tunamtaka kiongozi, wa kutuongoza na kutuelekeza, ili tuelekee kwenye maendeleo.

Urais, si nafasi ya kuwapenda rafiki na ndugu au kuwatafutia ndugu kazi. Si nafasi ya kufanya sherehe na kuzungukwa na rafiki, ndugu na jamaa. Haitoshi kuwa mtu mwema, kuwa na upendo na kuwa mcha Mungu. Kuna karama nyingi zinahitajika. Karama ambazo si kila mtu anazo. Ni bahati mbaya kabisa kwamba hapa kwetu Tanzania, kila mtu anafikiri anaweza kuwa rais. Kila mtu anafikiri anaweza kuwa kiongozi. Hii si kweli, maana uongozi pamoja na kisomo na mambo mengine mengi ni karama. Na karama hii si ya watu wote.

Tulishuhudia kwenye uchaguzi wa 2015, jinsi watu wengi walivyojitokeza kugombea nafasi moja tu ya urais wa taifa letu. Mbali ya watia nia wa vyama vingine, tulishuhudia watu zaidi ya 40 wa CCM wakitaka kuteuliwa na chama chao ili kugombea nafasi ya urais. Kila mtu, anafikiri na kutamani kuwa rais. Si kweli kwamba kila mtu ana sifa na uwezo wa kuwa rais. Labda hata leo hii bado ndugu yetu Lowassa, bado ana ndoto za kuwa rais wa taifa letu la Tanzania.

Binafsi niko mbali na mawazo kwamba Ikulu ya Tanzania, ni lazima ikaliwe na “wenyewe”. Siko huko, maana imani yangu ni kwamba Tanzania ni yetu sote na kila Mtanzania, anaweza kuingia Ikulu. Hatuna uongozi wa Kifalme, hapa, hivyo sitegemei Ikulu yetu kuwa na wateule fulani. Ikulu yetu haina chama na wala hakuna chama kilichoandikiwa kuwa Ikulu milele. Hoja yangu ni kumliganisha Lowassa, na wazee waliomtangulia. Namwangalia huyu ndugu yetu asiyechoka kuitamani Ikulu.

Huyu ni kati ya watu waliozipigania sekondari za kata. Kwa nini asipambane bila kuchoka na kuhakikisha sekondari hizi zinaendelea vizuri? Huyu ni mtetezi wa wafugaji, yeye mwenyewe ni mfugaji; kwa nini asipambane bila kuchoka ili kuhakikisha wafugaji wanapata haki zao na wanafuga kisasa?

Ni lazima apambane bila kuchoka kuingia Ikulu? Kwa nini safari yake ya kuingia Ikulu ni ya udi na uvumba, kufa na kupona? Ni lazima tujiulize. Alishindwa CCM, akakimbilia Ukawa. Kwa nini?

Lowassa, ameonja kwa namna yake kupanda na kushuka na kupanda, katika siasa za Tanzania. Alipokuwa Waziri wa Ardhi, jina lake lilivuma Tanzania nzima. Kila mtu alimfahamu na kumpenda. Alimwagiwa sifa nyingi za ushujaa na utetezi wa haki ya wanyonge. Mwalimu Nyerere, kwa sababu zake alizozifahamu alilishusha jina Lowassa. Na mwanzoni mwa Serikali ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa, ilimtupa kapuni. Baadaye aliibuka tena na kuingia kwenye Baraza la Mawaziri. Yaliyofuata hapo tunayafahamu wote, jinsi alivyovuma tena na kutengeneza mtandao wa nguvu hadi kupata nafasi ya uwaziri mkuu. Richmond ilishusha tena jina lake.

Huyu kwa tabia yake ni mpambanaji asiyechoka. Hapana shaka kwamba pamoja na kuonyesha kuchoka kimwili, bado ana nguvu za wafuasi. Bado ana watu wengi; wako kimya lakini wanamuunga mkono chini kwa chini na kimyakimya. Hatuwezi kumpuuza.

Bahati mbaya kuna wale wenye imani kwamba wao walizaliwa kuitawala Tanzania, ndoto za hivi ni za kizamani. Ndoto za sasa ni zile zinazopimwa na uzalendo wa mtu, hekima, busara, ubunifu, uelewa wa mtu juu ya demokrasia na utawala bora, usawa wa kijinsia na haki za binadamu, uelewa wa mtu juu ya mambo ya kitaifa na kimataifa, uwajibikaji na kisomo.

Hivi na vigezo vingine vingi vinatumika kumpima mtu mwenye sifa za kuwa kiongozi wa juu katika taifa.

Bahati mbaya, kuna wanaochanganya ubora wa kuongoza nchi na uzuri au ubaya wa mtu. Kipimo cha uzuri na ubaya wa mtu anacho Mungu peke yake. Afya ya mtu na miaka yake ya kuishi hapa duniani, anaijua Mungu peke yake. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kutambua na kuhukumu uzuri au ubaya wa mtu. Mimi na wengine wengi wanaojali, tunajaribu kuwachambua watia nia kwa vigezo muhimu.

Tunajaribu kuwapima wagombea kwa kazi zao za nyuma, maisha yao, matumaini yao na malengo yao ya mbele. Ni kitu gani kinawasukuma kutaka kuliongoza taifa la Tanzania. Ni ndoto na tamaa ya siku nyingi ya kufa na kupona au ni kusukumwa na hitaji la leo la kuwa na kiongozi bora wa kuliongoza taifa letu?

Kwa vile hili ni jambo la wazi na muhimu kwa taifa letu, hatuogopi kusema waziwazi kwamba mtu fulani hafai kwenye nafasi hii ya uongozi wa juu katika taifa letu. Kama mtu anasukumwa na hitaji la moyo wake la kufa na kupona, iwe na isiwe ni lazima awe rais wa Tanzania, mtu huyo hatufai. Haina maana kwamba kama mtu huyo hafai kwenye nafasi ya urais, basi hafai kabisa kwa mambo mengine. Inawezekana anayaweza mengine, lakini uongozi wa juu hapana.

Tunapoongelea ubora wa mgombea hatuna maana ya mvuto wa sura yake au uzuri wa aina nyingine: kuwasaidia watu, kuwafariji, kuwapatia misaada mbalimbali na kuwatendea wema wa kila aina. Inawezekana kabisa mgombea mwenye roho mbaya akawa kiongozi mbaya. Lakini pia inawezekana mgombea mwenye roho nzuri akawa kiongozi mbaya; huruma kupita kiasi, kushindwa kuwawajibisha wenye makosa kwa kuwahurumia na kuendeleza roho yake nzuri. Anaweza kuwa kiongozi mbaya kwa kushindwa kufanya maamuzi magumu kwa kisingizio cha “roho” nzuri.

Ubora wa kiongozi ni kuwa na mwelekeo, kuwa na msimamo, kufanya uamuzi mgumu, kuyafahamu vizuri matatizo na matumaini ya wale anaowaongoza. Ubora wa kiongozi ni kuwa na uwezo wa kuwaunganisha wale anaowaongoza. Ni wazi kuna zile sifa za jumla za uzalendo, uaminifu, busara, hekima na mchamungu.

Tunakumbuka Mwalimu Nyerere, aliorodhesha sifa za kiongozi ambaye taifa letu linamuhitaji nyakati hizi. Na kwamba pamoja na sifa zote hizo, awe ni mtu anayeona ufa kwenye msingi wa taifa letu.

Ufa huu umejitokeza katika maisha ya siku kwa siku kwenye taifa letu: Rushwa, ufisadi, makundi, matabaka, udini, ukabila, ubaguzi, ufa mkubwa kati ya maskini na matajiri na kuzika Azimio la Arusha.

Mwalimu, alipotaja ufu, kusema ukweli ufa huu, haukuwa mkubwa hivyo. Leo hii ufa huu ni mkubwa na kuna kazi kubwa mbele yetu. Pamoja na jitihada kubwa za Rais Magufuli, bado ufa huu unaonekana. Hivyo mfuasi wake ni lazima aweze kuona ufa huu pia na kuufanyia kazi.

Bahati mbaya wengi wetu tunashindwa kuona kazi kubwa iliyo mbele yetu. Badala ya kutulia na kuwachambua wagombea wetu kwa vigezo, tunakubali kutawaliwa na ushabiki wa uzuri na ubaya wa wagombea. Tunakubali kuingia kwenye mtego wa ushabiki wa vyama vya siasa.

Vyama vyote vya siasa vina matatizo, ingawa matatizo haya yanazidiana, lakini yanafanana. Uchu wa madaraka, upendeleo, rushwa, matumizi mabaya ya fedha za vyama na ushabiki wa kijinga. Tofauti hapa tunaangalia mwelekeo, msimamo, kuyafahamu matatizo ya taifa letu, kuwaunganisha Watanzania na kupambana kujenga uchumi wa kati wa taifa letu.

Huu ndio msingi wa kumpima kila mgombea wa urais wa taifa letu na rafiki yetu Lowassa, hawezi kukwepa msingi huu kama bado anatamani kuiingia Ikulu.

Padre Privatus Karugendo.

+255 754 633122