Lema amshauri JPM kuruhusu maandamano

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema

Muktasari:

Akizungumza katika mkutano wa hadhara Kata ya Murieti jana, Lema alisema Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa kwa kuruhusu watu wanaompinga kwa tuhuma za kuiba kura kuandamana na kuwapa ulinzi wa polisi.

Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amemshauri Rais John Magufuli aruhusu mikutano ya hadhara na maandamano.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara Kata ya Murieti jana, Lema alisema Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa kwa kuruhusu watu wanaompinga kwa tuhuma za kuiba kura kuandamana na kuwapa ulinzi wa polisi.

Katika uchaguzi wa Kenya, Kenyatta alitangazwa mshindi dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga aliyekuwa anaungwa mkono na muungano wa upinzani wa Nasa ambaye amekwenda mahakamani kupinga ushindi huo.

Alisema kuruhusiwa kwa maandamano na mikutano kuna faida kwa pande zote kwani chama tawala kitajua hisia na malalamiko ya upande wa upinzani na kuzifanyia kazi, lakini pia vyama vya upinzani vitakuwa vinatimiza wajibu wake wa kuzungumza kwa uhuru na wananchi.

Alisema suala la demokrasia linatazamwa katika nyanja mbalimbali akisema wawekezaji wakubwa wanakwenda katika Taifa ambalo ni tulivu kidemokrasia.

Akizungumzia vita dhidi ya ufisadi inayoendelea nchini, Lema alisema ni muhimu Rais Magufuli kutambua kuwa anapambana na mfumo ambao umeasisiwa na chama tawala, hivyo anapaswa kujenga mfumo ambao hata kama akiondoka, Taifa halitarudi lilipotoka.

“Tunapaswa kujenga mfumo imara ili kiongozi yeyote akichaguliwa kuliongoza Taifa hili, aweze kuufuata,” alisema

Shamba la Sumaye

Akizungumzia sakata la waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kunyang’anywa mashamba yake, Lema alisema ni uonevu na ukiukwaji wa utawala bora kwani si kweli kuwa waziri mkuu hiyo mstaafu hayaendelezi.

Lema alisema shamba la mke wa Sumaye alilonyang’anywa na Serikali kwa madai ya kutoliendeleza mkoani Morogoro lina mifugo na kuliendeleza kwake ni kuacha nyasi na si kujenga nyumba.

“Unapokuwa na shamba la mifugo, uendelezaji wake ni kuacha nyasi nyingi kuota kwani ndiyo malisho ya mifugo. Sasa huwezi kusema shamba la mifugo halijaendelezwa kwa kuwa ni pori,” alisema.

Awali, Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema ofisi yake itaendelea kuboresha huduma muhimu kwa wananchi akisifu kazi inayofanywa na watendaji kwa kushirikiana na madiwani.

Alisema ujenzi wa barabara za lami katika jiji la Arusha ni sehemu ya mipango iliyopitishwa na madiwani hao sambamba na mingine inayoendelea.