Lema amshukia Mambosasa kwa mdai ya kutengeneza ‘sinema’ ya kutekwa ‘Mo’ Dewji

Muktasari:

  • Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema amesema Kamanda wa Polisi Jijini Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ametengeza ‘sinema’ nyingine kuhusu tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’

Dodoma. Sakata la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ limeibuka kwa namna nyingine bungeni ambapo Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ametengeneza ‘sinema’ nyingine katika tukio hilo.

Akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa  Maendeleo wa mwaka 2019/20 jijini hapa leo, Lema alisema jana Jumapili aliona a sinema nyingine ya Mambosasa.

“Mheshimiwa nimeiangalia kwa makini ile sinema, unashindwa kuelewa ni mtoto wa namna gani anadanganywa. Yule bwana anayesema kuwa ndiye aliyewapangishia nyumba wale watekaji.”

“Yule bwana kwenye picha anaonekana ni rafiki yake Dk shika,  mmeenda kutafuta Dk Shika mwingine kutengeneza sinema nyingine ya ajabu ajabu. Watu wanaona huyu Mo aliyetekwa anajua alipokuwa anaweza asituambie sisi lakini akawaambia ndugu zake,” alisema.

Alisema kufuatia tukio la kutekwa ‘Mo’ kuna watu wapo kwenye biashara ambao wanasubiri baadhi ya masuala yao yakamiliki ili waondoke nchini.

Alisema biashara katika machimbo ya madini ni mbaya na kwamba hakuna utulivu wa kisiasa nchini.

“Mataifa ya nje kila siku yanatoa ‘articles’ kuhusu Tanzania siyo salama ya kuwekeza na majibu yake yanavyojibiwa yanajibiwa kihuni,”alisema.

Alisema kitendo cha bilionea kutekwa na Mambosasa kuja na picha za kamera ya kawaida kinawatia hofu wafanyabiashara.

 “Ili uweze kuwa na nguvu unahitaji ujasiri katika taifa hili mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya anaweza kuwa na sauti kuliko mawaziri. Leo hii tumeona taarifa za wakuu wa mikoa wakifanya unyanyasaji  kwa wawekezaji.”

“Dc (mkuu wa wilaya) anasema mweke huyu mwekezaji ndani masaa 48 watu

wanaona. Mheshimiwa mwenyekiti hawa (mawaziri na makatibu tawala) wanaanza kukosa heshima,” alisema.

Mbunge huyo alisema wafanyabiashara wanafunguliwa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha na kwamba wakiwa mahabusu wanafika watu ambao wanawataka watoe kiasi cha fedha ili waachiwe.

Alisema kuna msemo kuwa watu waishi kama mashetani lakini kama wataishi kama mashetani wengine wataishi kama watoto wa mashetani na kuishauri  Serikali kujenga ujasiri kwa wafanyabiashara ili waweze kujenga nchi.