Lema atakiwa kujisalimisha polisi Arusha

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema

Muktasari:

  • Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ametakiwa kujisalimisha kituo kikuu cha Polisi mkoani Arusha leo Jumapili Oktoba 21, 2018

Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ametakiwa kujisalimisha kituo kikuu cha Polisi mkoani Arusha leo Jumapili Oktoba 21, 2018.

Akizungumza na MCL Digital leo jioni Lema amesema ametakiwa popote alipo afike polisi kabla ya nguvu kutumika kumsaka.

"Hivi sasa nipo njiani natokea Moshi kuelekea Arusha. Nimetakiwa kuripoti polisi hata kama ni usiku na sijaelezwa kuna tatizo gani," amesema.

Kabla ya kuzungumza na MCL Digital Lema kupitia ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter aliandika juu ya kutakiwa polisi.

“Nimepigiwa simu na Polisi kwamba natakiwa kuripoti kituo kikuu cha Polisi Arusha leo bila kukosa, sijaelezwa sababu lakini wito unaonekana kuwa wa lazima sana, lakini nafikiri kupigania haki ndio linaweza kuwa kosa langu kubwa. Msiogope,” ameandika

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng'azi amesema taarifa za kuitwa Lema zitatolewa, “Kama anasema amepigiwa simu na yupo njiani anakuja basi akifika  tutajua."

Amesema ofisi ya Kamanda ni taasisi hivyo taarifa kamili zitatolewa baada ya Lema kufika kama alivyoeleza.