Lema hoi kwa kutokula

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema

Muktasari:

  • Mwanasheria wa mbunge huyo, John Malya amesema hali ya mbunge huyo si nzuri

Arusha. Hali ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliyeko mahabusu jijini hapa tangu alipokamatwa na polisi Ijumaa iliyopita, inadaiwa kuwa ni mbaya baada ya kugoma kula akishinikiza kupelekwa mahakamani.

Mwanasheria wa mbunge huyo, John Malya amesema hali ya mbunge huyo si nzuri, huku akisisitiza kuwa kama asipopelekwa mahakamani mpaka kufikia leo saa tano asubuhi, wataandika barua Mahakama Kuu, ili itoe agizo kwa polisi kumpeleka mahakamani.

Tangu mbunge huyo alipokamatwa akiwa nyumbani kwake, amegoma kula huku akishinikiza kupelekwa mahakamani.

Awali, Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alimkariri mbunge huyo akisema yuko tayari kufa kwa kutokula kama ataendelea kuwekwa mahabusu.