Lipumba amshambulia Maalim Seif, Chadema

Muktasari:

Lipumba alitoa tuhuma hizo jana, wakati wa kongamano la Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), lililofanyika kwenye ofisi za chama hicho Buguruni.

Sarakasi zimeendelea ndani ya Chama cha CUF baada ya mwenyekiti wake anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kumshutumu Maalim Seif Sharif kwa madai ya kutaka kukiua chama hicho.

Lipumba alitoa tuhuma hizo jana, wakati wa kongamano la Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), lililofanyika kwenye ofisi za chama hicho Buguruni.

Akihutubia kongamano hilo alimtuhumu Maalim Seif kwa madai ya kubadili utaratibu wa vikao vya ushauri kwa kuzungumza na mkurugenzi mmoja mmoja badala ya kuwaweka pamoja.

Alisema kitendo hicho ni cha kumdhalilisha Naibu Katibu mkuu wa chama hicho Bara, Magdalena Sakaya.

“Sakaya amefanya kazi kubwa sana kukijenga chama hiki. Lakini leo katibu mkuu (Maalim Seif) anamsimamisha uanachama Sakaya ili afukuzwe ubunge. Hivi tunajenga chama kweli hapa,” alihoji Lipumba na kujibiwa na wanachama wenzake kuwa chama kinabomoka.

Alisema huu ni wakati wa kukijenga chama na hakuna mwanasiasa bara aliyefanya kazi kubwa kuwatetea Wazanzibari kama yeye (Lipumba).

“Nasikia Maalim Seif anasema kutatokea machafuko endapo Rita wakifanya mambo yao. Maalim…hivi kukiwapo maandamano, kweli utakuwa mstari wa mbele, lini kulitokea ukawapo? Wakati maandamano yakifanyika unakimbilia Ulaya na habari unazipata huko huko,” alisema Lipumba.

Hata hivyo, Lipumba alisema amemsamehe Maalim Seif na yupo tayari kukaa naye meza moja ili kukijenga chama hicho ikiwamo kujenga uchumi utakaoleta manufaa kwa wananchi.

“Wakati wowote Maalim Seif njoo tuzungumze na turekebishe mambo,” alisema Lipumba.

Pia, Lipumba alikishutumu Chama cha Chadema kwamba kinamhadaa Maalim Seif na kinaweza ‘kumuuza’ kama kilivyofanya kwa Dk Wilbrod Slaa na kwamba hakina demokrasia kama kinavyotamba.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalim alisema chama hicho kinamtakia kila la kheri Lipumba na alimtaka akiache chama hicho kama kilivyo.

“Hata kama …hatuna demokrasia atuache kama tulivyo. Lakini tunachojua hatumtambui yeye kama mwenyekiti wa CUF,” alisema Mwalim.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema Lipumba bado anaendelea kutapatapa na asitarajie yeye au Maalim Seif kufanya naye kazi pamoja.

“Umeniambia Profesa Lipumba amemsamehe Maalim Seif kwa kosa lipi? Hivi kati yake na Maalim nani kafanya kosa. Profesa Lipumba ndiyo anatakiwa kuomba msamaha Watanzania,” alisema.

Alisema chama hicho kinafuata taratibu na hatua ya kumsimamisha uanachama Sakaya ilifuata kanuni kwa mujibu wa chama hicho.

Profesa Lipumba aliingia katika mgogoro na chama chake baada ya kuandika barua ya kujivua uenyekiti lakini baada ya mwaka mmoja wa nje ya uongozi alitengua kujiuzulu kwake.

Mkutano mkuu wa chama hicho ulikubali barua ya Lipumba ya kujiuzulu uongozi, lakini baadaye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini iliandika barua ya kumtambua Lipumba kuwa ndiye mwenyekiti halali wa CUF, hali iliyokipasua chama hicho hadi sasa.