Lipumba amuhofia Maalim Seif

Muktasari:

“Kwa muda mrefu tangu Septemba 23, 2016 nimekuwa natoa wito kwa katibu mkuu aje ofisini Buguruni nimpe maelekezo ya ujenzi wa chama chetu. Nimemuandikia memo na kumtumia barua pepe lakini mpaka leo hajafika licha ya kuwa makazi yake yako Mtaa wa Sharif Shamba, Wilaya ya Ilala jirani na ofisi kuu, Buguruni.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemshutumu Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kwamba anawatisha wajumbe wa ngazi mbalimbali za chama hicho.

“Kwa muda mrefu tangu Septemba 23, 2016 nimekuwa natoa wito kwa katibu mkuu aje ofisini Buguruni nimpe maelekezo ya ujenzi wa chama chetu. Nimemuandikia memo na kumtumia barua pepe lakini mpaka leo hajafika licha ya kuwa makazi yake yako Mtaa wa Sharif Shamba, Wilaya ya Ilala jirani na ofisi kuu, Buguruni.

 “Hivi sasa na mimi nimebaini wazi kuwa katibu mkuu hana nia ya kujenga CUF imara Tanzania Bara. Vitendo vyake ni mwendelezo wa imani na dhamira yake ya kuwapo kwa Muungano wa mkataba kama alivyotoa maoni yake binafsi kwenye Tume ya Jaji Warioba,” amesema Profesa Lipumba.

Mgogoro katika chama hicho ulishika kasi mwishoni mwa mwaka jana baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti halali wa CUF, wakati alishatangaza kujiuzulu nafasi yake kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 jambo lililosababisha kukigawa katika makundi mawili.