Lipumba amwaga ‘sumu’ Pemba, Mazrui amjibu

Muktasari:

  • Akizungumza katika mkutano wa ndani wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Makonyo Chake Chake Pemba, Profesa Lipumba alisema nguvu ya CUF haipo tena kwa sababu hakipo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa amesema chama hicho hakina nguvu visiwani Zanzibar kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma kwa sababu ya uamuzi mbaya kiliouchukua wa kususia uchaguzi wa marudio.

Akizungumza katika mkutano wa ndani wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Makonyo Chake Chake Pemba, Profesa Lipumba alisema nguvu ya CUF haipo tena kwa sababu hakipo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Alimtuhumu Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa chanzo kwa uamuzi wake wa kubariki kutoshiriki uchaguzi huo, jambo lililokifanya kikose sifa za kuwamo katika serikali hiyo.

Wakati Profesa Lipumba akieleza hayo, Nassor Ahmed Mazrui ambaye ni naibu katibu mkuu wa CUF Zanzibar upande unaomuunga mkono Maalim Seif, alisema hawatambui ziara hiyo kwa maelezo kuwa mwenyekiti huyo si kiongozi wao.

“Chama kinawataka wanachama, viongozi na wapenzi wa CUF waliopo Pemba na Unguja kuwa watulivu na kuendelea na shughuli zao za maisha ya kawaida na kupuuza kabisa ujio huo wa Profesa Lipumba,” alisema Mazrui.

Mazrui alisema CUF kipo imara na hakijaishiwa nguvu kama Profesa Lipumba anavyodai.

“Mimi ndiyo mtendaji wa shughuli za chama, mwezi uliopita nilifanya tathmini inayoonyesha CUF ina nguvu na bado ipo imara. Pia wanachama na wafuasi wake wanakikubali na wana morali,” alisema Mazrui.

Januari 28, 2016 Baraza Kuu la Uongozi la CUF lilitangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi (ZEC), likitoa hoja 12 za uamuzi huo.

Uchaguzi huo wa marudio wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani ulifanyika Machi 20, 2016.

Uamuzi huo wa CUF kutoshiriki uchaguzi huo ulitokana na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani uliofanyika Oktoba 25, 2015 kwa maelezo kuwa sheria na kanuni zilikiukwa na baadaye kutangaza kurudiwa upya.

Kususia kwake kushiriki, kulikipa fursa CCM kushinda kwa kishindo uchaguzi huo huku Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akiwateua wanachama wa vyama vingine vya upinzani katika baraza lake la mawaziri, akiwamo, mlezi wa chama cha ADC Hamad Rashid Mohamed ambaye pia aliwania urais kupitia chama hicho aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.

Katika mkutano wake wa jana, Profesa Lipumba alisema CUF kuwapo ndani ya SUK ilikuwa ni fursa kubwa kwake kupiga hatua za maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla na kwamba kukosekana kwake kumewanyima haki wananchi wanaokiunga mkono.

“Wawakilishi wangapi tumekosa kwa kugomea uchaguzi? Nataka ieleweke kuwa mtu akifanya jambo lazima aangalie masilahi ya mbali badala ya kuangalia masilahi ya karibu,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema hatua hiyo inaweza kutoa mwanya kwa chama tawala kubadilisha Katiba kwa urahisi kwa sababu SUK haipo.

Pia Profesa Lipumba alisema matukio mengi yakiwamo ya kupigwa kwa wafuasi wa CUF hasa katika maandamano yaliyofanyika miaka ya nyuma yanatokana na Maalim Seif kutofuata maelekezo ya viongozi wenzake wa juu wa chama hicho.

Mbali na hilo, Profesa Lipumba aliwakumbusha wanachama na wafuasi wa chama hicho waliohudhuria mkutano huo namna aliyojiuzulu Agosti, 2015 na kurejea katika nafasi hiyo mwaka mmoja baadaye.

Profesa Lipumba ambaye pia mtaalamu wa uchumi, aliwasomea wajumbe hao barua yake ya kujiuzulu wadhifa huo na ile ya kutengua uamuzi wake huo.

Aliwaambia wana CUF hao kuwa hivi sasa si wakati wa kulumbana, bali ni wa kuunganisha nguvu ili chama hicho kiendelee kudumu na kutetea haki za wanachama na wananchi.

Akijibu hoja kususia uchaguzi, Mazrui alisema mazingira yaliyojitokeza katika Uchaguzi wa Mkuu 2015, chama hicho kisingiweza kushiriki uchaguzi wa marudio.

“Hatuyumbishwi, hatujutii kutoshiriki uchaguzi ule, bali tunasonga mbele ya kudai haki yetu ya Oktoba 25, 2015,” alisema.

Mazrui alisema hawakushangaa kusikia Profesa Lipumba akitoa kauli hiyo dhidi ya CUF upande wa Zanzibar na kusisitiza kwamba uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi uliamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi Taifa la chama hicho.

“Tunawajua watu waliopo nyuma ya ziara hii ya Profesa Lipumba na waliofanikisha mpango huu.Ndio maana hatutambui ujio wake na hatuna shida wala hatuhitaji kusikia maneno yake,” alisema Mazrui.

Mmoja wa viongozi waliokuwamo katika kikao hicho cha Lipumba ni mbunge wa zamani wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa ambaye aliwataka wanachama wa CUF kuamka na kuachana na tabia ya kumfanya Maalim Seif kama mfalme katika chama hicho.

“Licha ya upendo mlionao kwa Maalim Seif, lakini mtambue wakati wa kufanya hivyo umepita hasa kwa sababu ameshawambia uongo na anaendelea kuwadanganya,” alisema.

Kauli ya polisi

Akizungumzia ziara ya Profesa Lipumba juzi, kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Shekhan Mohamed Shekhan alisema anayo taarifa,
“Ni kweli tumepokea taarifa ya ujio wake na tutatoa ulinzi kwa maana anatambuliwa na vyombo husika kama kiongozi ukizingatia zaidi mazingira walionayo kwenye chama chao.”

Mgogoro CUF

Mgogoro CUF ulianza mwaka 2016 baada ya Lipumba aliyekuwa amejiuzulu kutengua uamuzi huo. Alitangaza kujiuzulu uenyekiti, Agosti 5, 2015 lakini baada ya mwaka mmoja alitengua uamuzi huo na kurejea katika wadhifa huo jambo ambalo lilipingwa na baadhi ya wananchama.

Mgogoro huo umezaa makundi mawili ya wanachama, moja linaloongozwa na Profesa Lipumba na jingine, Maalim Seif. Mgogoro huo umesababisha pande hizo mbili kuburuzana mahakamani.