Lissu, Lowassa wazua jambo Bavicha, UVCCM

Muktasari:

Juzi, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka anadaiwa kusema kuwa Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema ni muongo kwa kuwa yeye si mwanasiasa wa kwanza kupigwa risasi huku akiwataja baadhi ya viongozi waliouawa kwa kupigwa risasi.

Dar es Salaam. Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) limekasirishwa na kauli iliyotolewa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) baada ya umoja huo kumshukia Mbunge wa Singida Kaskazini, Tundu Lissu kuwa ni mwongo na mpotoshaji.

Juzi, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka anadaiwa kusema kuwa Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema ni muongo kwa kuwa yeye si mwanasiasa wa kwanza kupigwa risasi huku akiwataja baadhi ya viongozi waliouawa kwa kupigwa risasi.

Kauli hiyo ilikuja baada ya Lissu kuzungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Nairobi, Kenya kwamba kabla na baada ya uhuru Tanzania haijawahi kushuhudia mwanasiasa akishambuliwa kwa risasi katika mazingira yaliyomtokea.

Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7 mwaka jana katika makazi yake mjini Dodoma akiwa anatokea bungeni. Alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Dodoma (General) baadaye kuhamishwa Hospitali ya Nairobi alikopatiwa matibabu kwa miezi minne kabla ya kupelekwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita alisema kauli ya Shaka inapaswa kukemewa na wapenda amani wote.

“Hata kama kweli Lissu sio mwanasiasa wa kwanza kupigwa risasi je, mambo haya hatupaswi kuyakemea katika nchi yetu?” alihoji

Alisema Shaka kwa kauli yake anaonyesha kuwa anafurahia vitendo vya kinyama kuendelea kutokea na anawajua waliomshambulia Lissu.

“Shaka amejuaje kama waliomshambulia Lissu hawakuwa na sababu za kisiasa, anafurahia vitendo hivyo?” alisema.

Alisema ikiwa Serikali imekataa kumjibu Lissu ikisema bado ni mgonjwa, Shaka anapata wapi ujasiri huo wa kujibizana naye.

Alimtaka Shaka akumbuke kwamba alichokizungumza Lissu ni kwamba hakuna kiongozi wa upinzani aliyewahi kupigwa risasi kama ilivyomtokea yeye.

“Tunamtaka Shaka aache kupotosha hoja zinazotolewa na viongozi wa Chadema kwani hazitamsaidia,” alisema.

Lowassa

Kuhusu kitendo cha Edward Lowassa kusifia utendaji wa Rais John Magufuli, Mwita alisema Bavicha imeshtushwa na kitendo hicho cha mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema.

Alihoji Lowassa anapata wapi ujasiri wa kumpongeza Rais wakati nchi inakabiliwa na matukio mengi ya uvunjaji wa haki za binadamu.

“Unampongezaje wakati Serikali yake bado haijatoa tamko lolote tangu mwanasheria wa Chadema Tundu Lissu alipopigwa risasi? Unampongeza vipi wakati Serikali imefuta mikutano ya vyama vya siasa?”

Mwita alisema kitendo cha Lowassa kumpongeza wakati vyama vya siasa vikiwa na malalamiko mengi kimewasikitisha hasa kutokana na mazingira ya siasa yalivyo hivi sasa hapa nchini.

“Vyama vya upinzani vina malalamiko mengi kwa Serikali, hatukutegemea kiongozi kama Lowassa asimame hadharani kumpongeza Rais Magufuli,” alisema.

Alipoulizwa iwapo Lowassa atahamia CCM chama hicho kitaathirika vipi, Mwita alisema hakuna cha kuhofia kwa kuwa wanachama wengi wanahama na hakitetereki.

“Lowassa akihamia CCM tutamtakia maisha mema kwani wako wengi wamehamia huko,” alisema.

Hata hivyo, alisema kwa sasa msimamo wa Bavicha ni kama ulivyo wa chama hicho uliotolewa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

“Tunasubiri vikao vya chama vitoe msimamo kuhusu jambo hili,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba Lowassa katika pongezi zake kwa Rais hakuwakilisha maoni ya chama hicho, bado suala hilo lina ukakasi.