Lissu ataka wananchi wasizuiwe kuzungumzia utekwaji wa Mo Dewji

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu 

Muktasari:

Tundu Lissu leo Jumanne Oktoba 16, 2018 amezungumzia tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ akitaka wananchi waachwe wazungumzie tukio hilo kwa maelezo kuwa kukaa kimya kutawafanya wanaoteka watu kuendelea kufanya hivyo


Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amezungumzia tukio la kutekwa mfanyabiashara maarufu nchini Mohammed Dewji 'Mo Dewji’ na kutaka wananchi wasizuiwe kuzungumzia matukio ya aina hiyo.

Lissu aliyeko nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 16, 2018 siku tano tangu mfanyabiashara huyo alipotekwa.

Mo Dewji alitekwa alfajiri ya Oktoba 11, 2018 katika Hoteli ya Colosseum Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kwa ajili ya  kufanya mazoezi.

“Hii habari ya kutekwa tusiingize siasa ni hoja ya hovyo kabisa maana yake ‘in practice’ ni kwamba tusiilaumu Serikali kwa mambo haya mabaya yanayotokea wakati kuna watu wametekwa na kupotea na hadi sasa kimya,” amesema Lissu.

“Ben Saanane  (msaidizi wa Freeman Mbowe-mwenyekiti wa Chadema), Azory Gwanda  (mwandishi wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi mkoani Pwani)  na  Michael Kanguye (mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko) wamepotea hawajulikani walipo.”

Ameongeza, “Kuna watu wametekwa nyara na kuteswa kama  wasanii Roma Mkatoliki, Ney wa Mitego, Mwanakotide wa Chadema. Hawa waliachiwa baada ya watu kupiga kelele.”

Lissu pia ametolea mfano tukio lililompata la kushambuliwa kwa risasi na kwamba tangu wakati huo hadi sasa mambo yamekuwa kimya, hakuna anayelizungumzia tena zikiwemo mamlaka husika.

“Sasa wamemteka nyara Mo Dewji mnataka tukae kimya ili tuwasaidiae watu kukaa kimya,” amesema Lissu.

“Ukimya unaua. Ukimya unawezesha wauaji na watekaji kuendelea kutenda maovu. Tusishiriki kwenye mauaji haya na utekaji huu. Tupige kelele tuokoe maisha ya Mo na wengine.”

Soma zaidi: