Lita 100,000 za maziwa ya Azam zakwama bandarini zikidaiwa ushuru wa forodha

Muktasari:

Taarifa zinaonyesha maziwa hayo yameadimika sokoni kwa zaidi ya mwezi.

Dar es Salaam. Baada ya maziwa ya Azam kuadimika mtaani, Serikali imesema inalishikilia shehena la kampuni ya S. S Bahressa kutokana na kudawa ushuru wa forodha.

Taarifa zinaonyesha maziwa hayo yameadimika sokoni kwa zaidi ya mwezi, baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushikilia zaidi ya lita 100,000 za maziwa hayo kutoka Zanzibar kutokana na kutolipiwa ushuru wa forodha.

Akitolea ufafanuzi suala hilo, kaimu mkurugenzi wa huduma za mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Martin Ruheta alisema mifugo na bidhaa zake yakiwamo maziwa si suala la Muungano na kwamba kampuni hiyo inapaswa kuyalipia kodi.

“Kuna mzigo wa Azam tumeuzuia mpaka utakapolipiwa kodi. Kwa muda mrefu (S. S Bahressa) walikuwa hawalipi baadhi ya tozo ila tunalishughulikia suala lao ili waendelee na biashara,” alisema Dk Ruheta.

Kiwanda cha maziwa cha kampuni hiyo kipo Zanzibar ingawa mauzo ya bidhaa zake hufanyika mpaka bara. Alisema tangu yalipoanza kusambazwa Bara, yalikuwa hayalipiwi ushuru wa forodha kwa mujibu wa sheria.

Dk Ruheta alisema mifugo na uvuvi inayoingia bara kutokea Zanzibar inapaswa kulipiwa ushuru wa forodha kama inavyofanywa kwa bidhaa kutoka nje ya nchi. Alisema mtu anayetaka kuingiza mzigo kutoka Zanzibar anapaswa kuomba kibali cha kufanya hivyo.

Pamoja na ukweli huo, aliwataka wananchi kutulia kwani suala hilo linashughulikiwa ili maziwa hayo yaendelee kusambazwa kama kawaida.

“Kuna mtalaamu wetu pamoja na mkurugenzi wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) wameenda Zanzibar, tunatarajia watatuletea majibu ndani ya siku tatu au nne zijazo yatakayotusaidia kupata muafaka wa suala hili,” alisema.

Wakati Dk Ruheta akisema hayo kwa niaba ya katibu mkuu wake, taarifa zinasema wataalamu wa kodi wa Azam wanafanya mawasiliano na viongozi wa Serikali kupata ufumbuzi wa kudumu wa uuzaji wa bidhaa zinazozalishwa pande mbili za Muungano.

Hata hivyo, msemaji wa kampuni za S. S Bahressa, Hussein Sufian alisema wanaendelea kuzungumza na mamlaka husika kupata suluhu.

“Ni mwezi sasa shehena hiyo inashikiliwa. Kuna utata kidogo,” alisema Sufian.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu suala la ushuru unaodaiwa na wizara, mkurugenzi wa elimu ya mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema hakuna maziwa yoyote ambayo yamekwamia kwao kutoka nje ya nchi au mahali pengine popote.

“Kwa rekodi zetu hakuna maziwa tunayoyashikilia. Kwa utaratibu uliopo, bidhaa kama hiyo ikiingia nchini ni lazima ipate kibali cha wizara husika kabla hayajalipiwa ushuru unaotakiwa,” alisema Kayombo.

Hii ni mara nyingine bidhaa kutoka Zanzibar zinakwama bandarini kwa madai ya ushuru wa forodha kwani mara kadhaa wananchi wamelalamika kuhusu kutozwa ushuru hata kwa bidhaa binafsi ambazo si za biashara.

Mwaka 2012 kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu ushuru unaotozwa kwenye magari yanayoingizwa bara kutokea Zanzibar kiasi cha baadhi ya wananchi kuona maofisa wa TRA wanataka kuwaibia katika ushuru huo.

Kutokana na ukweli huo, TRA walilazimika kuweka namba ya huduma kwa wateja ili kila mteja anayetaka kufahamishwa kuhusu ushuru huo aweze kuwasiliana na idara husika.

Licha ya magari hata wananchi walionunua runinga kutoka visiwani humo wamewahi kulalamika kwa nyakati tofauti kudaiwa ushuru wa forodha na maofisa wa mamlaka hiyo yenye dhamana ya kukusanya kodi ya Serikali.

Hivi karibuni, kiwanda cha Sukari cha Zanzibar kililalamika kunyimwa kibali cha kuuza zaidi ya tani 3,000 za sukari upande wa bara.

Uongozi wa kiwanda hicho ulieleza kushindwa kuuza sukari hiyo Zanzibar kwa sababu wanapata hasara ya Sh18,000 kwa kila mfuko wa kilo 50 wakitoa gharama za uzalishaji.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali alisema Serikali inaweka mikakati ya kuondoa changamoto zilizopo ili kufanikisha bidhaa hiyo kuuzwa bara ambako kuna soko kubwa kuliko visiwani humo.

Hali hiyo ilitokea wakati mahitaji ya sukari Tanzania yakiwa tani 590,000 kwa mwaka ilhali uwezo wa uzalishaji wa viwanda vya ndani ni tani 300,000 hivyo kuwa na upungufu wa tani 290,000 hivyo kulazimika kuagiza kutoka nje.