Lita 180 za damu zahitajika Kakonko

Muktasari:

  • Alisema kwa siku wastani zinatakiwa kuwapo lita sita kila kituo cha afya wilayani humo.

Kakonko. Mganga mkuu Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Dk Joseph Tutuba amesema mahitaji ya damu wilayani humo ni lita 180 kwa mwezi.

Alisema kwa siku wastani zinatakiwa kuwapo lita sita kila kituo cha afya wilayani humo.

Dk Tutuba alisema hayo juzi wakati wa uhamasishaji wananchi kujitokeza kuchangia damu katika uwanja wa mpira wa Kanisa Kuu Parokia ya Mtakatifu Therezia Kakonko, mkoani Kigoma. Alisema wilaya hiyo ina zahanati 26 ambazo uhudumia wagonjwa 123,000 kati ya hao, wanaohitaji damu ni kati ya 18,000 mpaka 20,000.

Mkuu wa wilaya hiyo, Hosea Ndagala alisema uchangiaji damu unaendeshwa na Redio Kwizera kutoka wilayani Ngara mkoani Kagera, viongozi na kuwataka wananchi kuunga mkono ili kuokoa maisha ya wagonjwa.

Naye mratibu uhamasishaji uchangiaji damu wa Redio Kwizera, Alex Mchomvu alisema walianzia Ngara, Manispaa ya Bukoba, Biharamulo, Karagwe na kupata lita 574.

(Shaaban Ndyamukama)