Lizer mwanaume nyuma ya ngoma kali za WCB

Lizer Classic

Dar es salaam. Siraju Hamisi huenda likawa jina geni kwako, lakini kama utaambiwa Lizer Classic inaweza kuwa rahisi kumtambua kutokana na kazi nyingi anazofanya na wasanii maarufu nchini. Wengi wameanza kumfahamu akiwa Wasafi Records, lakini safari yake kama wengine ilianzia mbali kidogo.

Katika mahojiano na Mwananchi, ameelezea hatua ya kwanza mpaka ya mwisho namna alivyoanza kufanya kazi na Wasafi Records ambapo ameweza kujipatia umaarufu kutokana na ubora wa kazi zake.

Anasimulia kwamba alianza kama mwimbaji wa Bongo Fleva akiwa mkoani Kigoma na ndipo lilipozaliwa jina la Star Lizer.

“Kikubwa kilichonifanya nijifunze utayarishaji wa muziki ni usumbufu wa hapa na pale nilipotaka kurekodi ngoma zangu, nikawaza siku moja kwamba kwa nini nisijifunze kutengeneza mwenyewe kwa kuangalia jinsi wanavyofanya, nikaanza mdogo mdogo mpaka nikaweza.

“Kutokana na kufahamika sana Kigoma kukafanya watayarishaji waniamini, wakati mwingine wakienda kula walikuwa wananiacha ndani na mimi sikuwa nyuma kutumia muda huo kujifunza namna ya kurekodi na kutengeneza biti mbalimbali,” anasema.

Anasema baadaye akapata uzoefu na kuanza kuwarekodia wasanii nyimbo na kuwatengezea biti, jambo lililozidi kumpa umaarufu mara dufu.

Safari ya kwanza ni Burundi

Kigoma na Burundi sio mbali, ilikuwa rahisi kwake kujulikana nchi hiyo kwamba ni mtayarishaji ndipo alipokea mwaliko kwa mara ya kwanza na mwimbaji wa nyimbo za injili ambaye alimuomba amtengenezee kazi zake.

“Kuna msanii wa nyimbo za injili kutoka Burundi alikuja katika Studio zetu pale Kigoma, alipenda kazi zangu alihitaji kufanya kazi na mimi lakini alitaka niende Burundi katika studio zao ambazo zilikuwa na vifaa vizuri zaidi.

“Nilipoenda Burundi nilimuandalia albamu nzima, ambapo mmiliki wa ile studio alipenda namna ninavyoandaa kazi na akanihitaji nibaki, basi nikaanza kupiga mzigo pale, nilifanya mambo makubwa yaliyowastaajabisha wengi.

“Kazi nilizofanya wakati huo ni sawa na sasa, ndivyo nilivyokuwa Burundi, wasanii wote wakali walikuwa wanakuja kufanya kazi na mimi,” anaongeza.

Haikuwa rahisi kumkubalia Diamond

Anasimulia namna alivyokutana na Diamond kwa mara ya kwanza, kuwa alifanya kazi naye kipindi ambacho staa huyo alikwenda kufanya shoo Burundi, ambapo alipata wasaa wa kushirikishwa katika kolabo na msanii wa nchini humo anayefahamika kwa jina la Lolilo na nyimbo ilikuwa inajulikana kwa jina la Natamani.“Ile kazi nilifanya mimi, kumbe Diamond alikuwa amependa sana namna sauti yake nilivyoitengeneza, alivyoanzisha studio alinitafuta ili nifanye kazi naye, lakini mimi nilimzingua,”

“Nilikataa kwa sababu sikuwa tayari kuondoka kule yaani ni sawa na sasa eti mtu aje aniambie nataka twende tukafanye kazi Kenya, kiukweli siwezi na ndivyo ilivyokuwa kwa Diamond nilimwambia kuwa nina mkataba, ukweli nilitumia busara kumkataa kiaina,” anasema.

Ilikuaje kubadili uamuzi?

“Wakati nikiendelea kufanya kazi kule, ilitokea kipindi ambacho hali ya kisiasa Burundi iliyumba, hivyo nikaamua kurudi nyumbani Kigoma.

“Wakati nikiwa Kigoma mambo ya Muziki kwa pale sikuyaelewa kabisa, ndipo nikakumbuka dili la Diamond nikaamua kumtafuta Q-Boy ambae nilikuwa nafahamiana naye kitambo ili awasiliane na Diamond kwani ndiye aliyemtumia wakati ananitafuta mimi.

“Bahati nzuri siku niliyomtafuta Q-Boy walikuwa pamoja na Diamond ambapo alimpokonya simu ikanipa urahisi wa kuongea naye moja kwa moja ndipo akanikumbushia ishu ya kufanya naye kazi, sikutaka kuremba tena ikabidi nimkubalie.

Alianza na Salome

“Nakumbuka wimbo wa kwanza kutengeneza ni Salome ingawa ulichelewa kutoka, naamini ulipokelewa vyema na wadau wa muziki nchini, ukafuatiwa na Harmonize, Bado, ukaja wa Rayvanny, Kwetu, hivyo ndivyo tunavyoendelea kufanya kazi kadri siku zinavyokwenda.

“Changamoto kubwa kufanya kazi na Diamond ni supastaa anayejulikana duniani kwa sasa, hivyo ninavyotengeza nyimbo zake lazima niweke umakini wa hali ya juu, ili isichuje haraka kwani yeye mwenyewe anaogopa kushuka.

“Mwanzoni nilikuwa namuogopa mpaka alikuwa ananiuliza au kazi zako ambazo nilikuwa nazisikia ulikuwa unafanyiwa, lakini nilipokuja kufanya ya Harmonize na Rayvanny akaja akaniamini na ndio mpaka sasa tunaendelea kufanya kazi.”

Harmonize alimpa makavu

“Ilifikia hatua Harmonize akaniambia mimi hamna kitu kwa madai sijiamini na akawa anamshawishi Diamond waanze kumtafuta mtayarishaji kutoka Nigeria, sasa kila kona walipokuwa wanasikia sifa ya wimbo ya ‘Kwetu wa Rayvanny ukafanya anibakishe na kuniamini.

Anasema ili mtayarishaji aonekane mzuri lazima awe na kitu kinachomtambulisha ama kumtofautisha na wengine.

Anaeleza kwamba kwa sasa anajiamini ana uwezo wa kufanya kazi na msanii yoyote nchini na kwamba ndoto zake alizotamani ziwe akiwa anaanza kazi hiyo zimetimia kwa asilimia 70.

Uwoga kwake kwa Rick Ross

“Nilipofanya biti ambalo Diamond alitakiwa kufanya na Rick Ross nilikuwa nina wasiwasi mkubwa kama je wataielewa maana wenzetu wako vizuri kwa vifaa na mambo mengine lakini nashukuru mambo yalienda vizuri.

“Diamond alirekodi huku alafu tukawatumia sauti ambapo Rick Ross akaingiza sauti yake, wakatutumia sauti mimi nikaimalizia kila kitu kuichanganya.

Kuhusu biti zake kufanana

“Produza yeyote lazima uwe na kitu chako ambacho ni kama utambulisho wako hivyo wanaosema mimi narudia biti kiufupi hawaujui muziki, maana msikilize mtayarishaji yeyote lazima kuna kitu chake cha utofauti utakuwa unakisikia kwa kila biti analotengeneza.

“Watu wanaongea sana kwamba wimbo wa Show Me na Kwangaru biti zake zimefanana, ila mimi huwa nawauliza kuwa nyimbo zimefanya vizuri au hazijafanya vizuri? Kama ndio basi kwangu huwa sijali hizo kelele,” anasema.

Anauwezo wa kutayarisha ngoma ngapi kwa siku

Anaongeza zaidi kua kwa siku anaweza kutayarisha nyimbo tatu huku muda wake wa kufanya kazi anapenda sana kufanya kazi kuanzia saa kumi usiku huku akitaja sababu kuwa kwake ndio muda ambao akili kwake inakuwa vizuri kwa kazi.

Nandy aliwahi kuwa Wcb.

“Wengi hawajui hili mwanzoni Nandy alikuwa hapa lebo lakini aliondoka nafikiri aliona muda kwake unachelewa kufanikiwa kutoka kimuziki akiwa hapa.

“Hata zile jingo mwanzoni wa wimbo unaosikia ukitoka Wasafi hapa au pale inapotaja jina la ‘eyoo Lizer’ ni yeye.

Kuhusu Lizer

Pamoja na kufaulu Shule ya Msingi, Lizer mwenye umri wa miaka 29 hakuendelea na masomo ya sekondari badala yake alijikita katika muziki.

“Nilisoma Shule ya Msingi Katubuka iliyopo Kigoma, nilipomaliza darasa la saba nilikataa kuendelea na masomo kitu ambacho kilisababisha nifukuzwe nyumbani,” anasema.

Anachojivunia katika muziki ni heshima aliyoijenga: “Muziki umenipa vitu vingi lakini kikubwa ninachoshukuru kukipata ni heshima,” anamalizia.