Lowassa, CUF wawalilia waliofariki dunia kuzama kwa MV Nyerere

Muktasari:

  • Wakati Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akituma salamu za rambirambi na kukosoa zoezi la uokoaji, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema ajali hiyo ni msiba kwa Taifa

Chama cha Wananchi CUF kimemtumia Rais John Magufuli salamu za rambirambi kufuatia kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere huku watu 94 wakiripotiwa kufariki dunia.

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ametuma salamu za rambirambi kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na chama hicho.

Katika taarifa hiyo, Maalim Seif alisema amesikitishwa kwake na uamuzi wa kusitishwa kwa shughuli ya uokoaji juzi jioni.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere (juzi) jana jioni, nampa pole zangu za dhati Rais John Magufuli, huu ni msiba wetu sote kama Taifa,” ilisema taarifa hiyo.

“Pia nawapa pole ndugu, jamaa na wapendwa wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hii Mwenyezi Mungu awape subra katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya kuondokewa na wapendwa wao.”

Kuhusu uokoaji, Maalim Seif alieleza kusikitishwa na kusuasua kwa uokoaji, hasa kitendo cha kusitishwa kwa muda ikielezwa ni kwa sababu ya kukosekana kwa taa na injini za boti.

 

“CUF inawataka viongozi wote wanaohusika na kadhia hii wakiwemo mawaziri wa wizara husika kuwajibika kwa kujiuzulu nafasi zao au kuwajibishwa na mamlaka za uteuzi wao kwa kutochukua tahadhari ya mapema,” alisema Maalim.

 

Chama hicho kimesema viongozi wa Serikali walipuuza tahadhari iliyotolewa na Mbunge wa Ukerewe (Chadema) Joseph Mkundi, wakikifananisha kitendo hicho na dharau.

Lowassa: Tujipange yasitokee tena

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alitoa salamu za rambirambi na kubainisha msiba huo ni wa Taifa.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na masikitiko makubwa taarifa za ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.” Alisema Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema

“Ninawapa pole ndugu wote waliopoteza maisha, mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Watanzania wote kwa ujumla.”

Lowassa alisema huu ni msiba wa nchi nzima huku akisema ni wakati wa kujipanga ili ajali kama hiyo isitokee tena. “Ni lazima tujiulize na kujipanga ili haya yasitokee tena.”