Lowassa: Kwa tume hii, CCM itatangazwa mshindi kila siku

Muktasari:

Badala yake, Lowassa ametaja mambo manne yanayotakiwa kufanyika ili kuwa na uchaguzi huru ikiwamo kuwa na tume huru ya uchaguzi.

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuendelea kuwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyopo sasa ni sawa na kufanya CCM iwe inatangazwa mshindi katika kila uchaguzi.

Badala yake, Lowassa ametaja mambo manne yanayotakiwa kufanyika ili kuwa na uchaguzi huru ikiwamo kuwa na tume huru ya uchaguzi.

Lowassa alikuwa akitoa maoni yake kuhusu uchaguzi mdogo wa majimbo ya Ukonga jijini Dar es Salaam na Monduli mkoani Arusha ambako wabunge wa CCM walishinda pamoja na madiwani wote 23 wa chama hicho tawala ulikofanyika uchaguzi mdogo sehemu mbalimbali nchini.

Akizungumza na Mwananchi jana, Lowassa alisema suluhisho la kuwa na uchaguzi huru ni kuwa na tume huru ya uchaguzi vinginevyo CCM itaendelea kutangazwa kuwa imeshinda katika kila uchaguzi.

“Kama hatuwezi kuwa na tume huru ya uchaguzi, CCM itakuwa inatangazwa imeshinda kila siku, kwa sababu sheria inasema anayetangazwa na tume ndiyo anakuwa ameshinda,” alisema Lowassa mara baada ya kutoka katika msiba wa mwanasiasa, John Guninita.

Alisema ili kufanya uchaguzi huo uwe wa huru na haki, lazima kuwe na sheria ambayo itafanya tume iwe inabanwa. “Lazima kuwe na chombo ambacho kinaibana tume, lakini sasa tume haiwezi kubanwa.”

Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa Monduli kwa miaka 25 tangu mwaka 1990 mpaka 2015, alisema jambo jingine ambalo linafanya uchaguzi huo kutokuwa huru ni kutokana na wakurugenzi na maofisa wanaosimamia uchaguzi huo kuwa wateuliwa wa Rais.

“Maofisa na wakurugenzi wanaosimamia uchaguzi, wanateuliwa na Rais na wana wajibu wa kumtii Rais,” alisema Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Awamu ya Nne.

“Wakurugenzi wengi walioteuliwa ni makada wa CCM ambao walianguka katika uchaguzi wa ubunge mwaka 2015, Rais akawateua, usitarajie kama wapo huru hao,” alisema.

Lowassa, ambaye alijiunga na Chadema Julai 28, 2015 siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu, alidai kuwa hata uchaguzi wa Jimbo la Buyungu ulipovurugwa msimamizi badala ya kuchukuliwa hatua alipandishwa cheo.

“Aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Buyungu alivuruga uchaguzi, siku ya pili akaja Dar es Salaam na kupandishwa cheo kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa Wilaya ya Temeke,” alisema Lowassa ambaye ametimiza siku 1,149 tangu aondoke CCM na kuhamia Chadema.

Lowassa alikuwa akimzungumzia aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Buyungu, Lusubilo Mwakabibi ambaye aliteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Temeke Agosti 13 katika uteuzi wa wakurugenzi wapya 41 wa halmashauri mbalimbali nchini.

Katika uchaguzi wa Buyungu uliofanyika Agosti 12, Christopher Chizza wa CCM alishinda lakini ubalozi wa Marekani nchini ulitoa taarifa ukisema uchaguzi huo mdogo ulikuwa na kasoro nyingi.

Lowassa ambaye aligombea urais kupitia vyama vilivyounda Ukawa na kupata kura 6,072,848 katika uchaguzi mkuu uliopita alisema wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ni watu muhimu katika chaguzi mbalimbali, lakini akahoji sifa zao.

“Wasimamizi na maofisa (wasimamizi wasaidizi) wa uchaguzi hawapo huru, wengi ni wafanyakazi wa Serikali, unatarajia uchaguzi utakuwa huru?” alihoji.

Lowassa ambaye pia amewahi kuwa waziri wa wizara mbalimbali, alishauri kuwa licha ya kuwa na tume huru, wasimamizi na maofisa wanaovuruga uchaguzi wawe wanashtakiwa kama ilivyotokea nchini Kenya.

Alitaka wanaofanya makosa katika uchaguzi huo wawe wanashtakiwa binafsi kutokana na makosa yao.

“Umeona Kenya, maeneo waliovuruga uchaguzi, wale maofisa na wasimamizi wameshtakiwa na sisi hapa tunapaswa kufanya hivyo,” alisema Lowassa.

Alipoulizwa kwa nini na wao wasiende mahakamani kama wanadhani kuna maofisa waliovuruga uchaguzi, Lowassa alisema, “Utaratibu wa hapa haupo vizuri, mchakato haupo vizuri kama kwa wenzetu.”

Baada ya kutangaza kuhama CCM, Lowassa alikuja na misemo mbalimbali na moja ya nukuu zake zilikuwa, “CCM si baba yangu wala mama yangu, Watanzania kama wameyakosa mabadiliko ndani ya CCM, basi watayapata nje ya CCM.”

Katika uchaguzi wa Jumapili iliyopita, msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Monduli, Stephen Ulaya alisema Julius Kalanga wa CCM alipata kura 65,714 sawa na asilimia 95 ya kura zote huku Yonas Laizer wa Chadema akipata kura 3,187.

Alisema walioandikishwa kupiga kura walikuwa 80,282 lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa 69,521.

Jimbo la Ukonga, msimamizi wa uchaguzi, Jumanne Shauri alimtangaza Mwita Waitara aliyepata kura 77,795 sawa na asilimia 89.19 kuwa mshindi wakati Asia Msangi wa Chadema akifuatia kwa mbali kwa kura 8,676 sawa na asilimia 9.95.

Alisema watu waliotarajiwa kupiga kura walikuwa 300,609 lakini waliojitokeza ni 88,270 sawa na asilimia 29.4.

Tangu kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015, zimefanyika chaguzi ndogo mara tano katika majimbo na kata mbalimbali, ambazo CCM imeshinda zote isipokuwa Kata ya Ibigi, Mbeya iliyochukuliwa na Chadema.