Lowassa: Msipingane na msimamo wa JPM

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amewashauri Watanzania wasipingane na misimamo ya Rais John Magufuli mpaka itakapofika mwaka 2020.

Muktasari:

  • Alisema wakati huo utafanyika uchaguzi mkuu na ndio wanaweza kufanya uamuzi.
  • Akihutubia viongozi wa chama hicho kutoka majimbo ya Muleba Kusini na Kaskazini jana, Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kupitia Chadema alisema wanachama hao waache kubishana naye hadi watakapokutana katika uchaguzi wa 2020.

Muleba/Bunda. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amewashauri Watanzania wasipingane na misimamo ya Rais John Magufuli mpaka itakapofika mwaka 2020.

Alisema wakati huo utafanyika uchaguzi mkuu na ndio wanaweza kufanya uamuzi.

Akihutubia viongozi wa chama hicho kutoka majimbo ya Muleba Kusini na Kaskazini jana, Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kupitia Chadema alisema wanachama hao waache kubishana naye hadi watakapokutana katika uchaguzi wa 2020.

Hata hivyo, Lowassa ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu, hakuitaja misimamo hiyo ya Rais Magufuli lakini tangu aingie madarakani, kiongozi huyo wa Awamu ya Tano ya Tanzania, ameweka msimamo mkali katika suala zima la kubana matumizi ya Serikali, kudhibiti watumishi hewa, safari za ndani na nje zisizo na tija na rushwa. Mambo hayo yamesifiwa na watu wengi.

Lowassa aliwaeleza viongozi hao kuwa uchaguzi wa mwaka 2020 unaweza kuwa rahisi zaidi huku akitaka wapinzani wapingwe kwa hoja na si kukandamizwa.

“Tupingane kwa hoja bila kuumizana na kutakiana mabaya, tuwasaidie wananchi wanaopata matatizo bila kuwapuuza,” alisema Lowassa.

Akizungumzia sababu ya kutembelea Mkoa wa Kagera, Lowassa alisema ni pamoja na kuwashukuru wananchi kwa kura walizompigia na kuwapa pole kwa tetemeko la ardhi lililowakumba Septemba mwaka jana.

Kada wa zamani wa CCM aliyeongozana na Lowassa, Hamis Mgeja, licha ya kujivunia kukihama chama hicho alisema kwa jinsi mambo yanavyokwenda, chama hicho tawala kinajifuta taratibu kwa wananchi.

Baadaye, Lowassa, alishiriki kampeni za kumnadi mgombea udiwani katika Kata ya Kimwani, wilayani Muleba.

Kuhusu uhaba wa chakula

Katika mkutano huo wa ndani, Lowassa alizungumzia hali ya ukame inayoikabili nchi na kusema kuna tishio kubwa la uhaba wa chakula hivyo kuitaka Serikali isipuuze majanga yanayoweza kuwapata wananchi, bali iwasaidie kwa kauli na vitendo.

“Wananchi wasipuuzwe, kuna tatizo la njaa kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, kwa hiyo wananchi wasaidiwe,” alisema Lowassa.

Wakati Lowassa akisema hayo Muleba, huko Bunda mkoani Mara, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimtaka Rais Magufuli kuchukua hatua kukabili hali ya upungufu wa chakula nchini.

Akihutubia mkutano wa ndani wa viongozi wa chama hicho Jimbo la Bunda Mjini uliofanyikia katika Hoteli ya Harieth, Mbowe alisema ni ukweli usiopingika kwamba taifa linakabiliwa na uhaba wa chakula, hivyo ni Rais Magufuli anapaswa akubaliane nao.

Mbowe aliyetumia takribani dakika 12 katika hotuba yake, alisema ukali anaouonyesha Rais kuhusiana na taarifa za uhaba wa chakula nchini unatia shaka.

“Awasikilize Watanzania waliomchagua kwani ndiyo waajiri wake. Wanaposema wana njaa awasikilize na kuwasaidia. Kuna uhaba wa chakula... hili halina ubishi. Ni wajibu wa Serikali kuchukua hatua za haraka,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema si kweli kwamba kuna uhaba wa chakula kutokana na uvivu wa wananchi kwani wengi ni wachapakazi isipokuwa wamefikwa na hayo yote kutokana na mvua kutonyesha kwa wakati.

“Njaa haijaletwa na uvivu wa Watanzania, bali imeletwa na ukame ambao uko nje ya uwezo wao,” alidai Mbowe.

Alizungumzia pia hatua ya Serikali kubana matumizi akisema imechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa Deni la Taifa, kampuni nyingi kufungwa, kushuka kwa mapato ya taifa na uwekezaji pamoja na umaskini miongoni mwa Watanzania na kumtaka alegeze.

Awali, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche kwa pamoja walimwelezea mwenyekiti huyo kuwapo kwa uhaba wa chakula mkoani humo na kumwomba alisemee.

Bulaya alisema wakazi wengi wa wilayani Bunda wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na ukame sambamba na mazao yao kuharibiwa na wanyama huku akisema watendaji wa Serikali hawataki kutangaza wakihofia kuondolewa kwenye nyadhifa zao.