Lowassa aishtukia Serikali ya CCM

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

Muktasari:

Lowassa, ambaye alikuwa mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM kabla ya kuhamia Chadema Julai mwaka jana, alisema hayo baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu hali inayoendelea mkoani Arusha kati ya viongozi wa Serikali na Chadema ambayo inaongoza Halmashauri ya Jiji.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema mgogoro unaozidi kukua baina ya viongozi wa mkoa na Chadema ni mpango wa Serikali kutaka kukatisha tamaa vyama vya upinzani ili visitekeleze majukumu yake kwa wananchi.

Lowassa, ambaye alikuwa mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM kabla ya kuhamia Chadema Julai mwaka jana, alisema hayo baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu hali inayoendelea mkoani Arusha kati ya viongozi wa Serikali na Chadema ambayo inaongoza Halmashauri ya Jiji.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na mkurugenzi wa jiji, Athuman Kihamia wameingia kwenye mgogoro na Chadema kutokana na wawili hao kuonekana kuingilia shughuli za Baraza la Madiwani linaloongozwa na Chadema kwa kutengua maamuzi yaliyowahi kufanywa na chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi.

Gambo alianza kuingia kwenye mgogoro na chama hicho wakati akiwa mkuu wa Wilaya ya Arusha, alipoagiza Takukuru ifanye uchunguzi wa ongezeko la posho za madiwani lililopitishwa na Katibu Tawala ya Wilaya, jambo ambalo Chadema ililipinga ikisema amevuka mipaka ya madaraka yake.

Gambo pia amefunga shule 48 za msingi ili akutane na walimu, kitu ambacho chama hicho kimesema ni kukiuka sheria.

Mkurugenzi wa Jiji naye ameingia kwenye mzozo baada ya kutangaza kufuta posho ya takrima ya meya ya Sh1.5 milioni akidai zitumike kulipa deni la Sh154 milioni bila ya kujadiliana na Baraza la Madiwani.

Pamoja na chama hicho kueleza kuwa sera yake ni kufuta posho zote za madiwani ili zitumike kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, kinapingana na maamuzi ya wawili hao kwa madai kuwa yanakiuka sheria na taratibu.

“Serikali inataka kukatisha tamaa vyama vya upinzani ili visitekeleze majukumu yake,” alisema Lowassa akiwa nyumbani kwake Monduli mkoani Arusha.

“Kinachoendelea mkoani Arusha ni mkakati wa Serikali kukandamiza upinzani na kuwakatisha tamaa ili wasifanikiwe katika majukumu yao.

“Serikali ya CCM inaumizwa kuona miji mikubwa, majiji na baadhi ya halmashauri zinaongozwa na vyama vya upinzani. Kwa hiyo wanachokifanya ni ku-frustate (kukatisha tamaa) ili wapinzani waonekane hawafai.”

Hata hivyo, Lowassa, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa), alisema mipango hiyo ya Serikali haitafanikiwa kwa kuwa wapinzani wamejipanga na wanajua wanachokifanya.

“Wanawatumia viongozi wao wa mikoa na wilaya ili tusifanikiwe, lakini sisi tumejipanga vizuri na wananchi wenyewe wanaona,” alisema Lowassa ambaye akiwa Waziri Mkuu alisimamia ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Chadema ni chama kikuu cha upinzani, ikiwa inashika nafasi ya pili kwa kuwa na wabunge wengi kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano na kuongoza halmashauri nyingi.

Pia, wapinzani kutokana na ushirikiano wa Ukawa ulioundwa na vyama vya CUF, NCCT Mageuzi na NLD, waliongeza idadi ya halmashauri ambazo kabla ya mwaka 2015 zilikuwa zikishikiliwa na CCM, huku ACT Wazalendo ikishika Halmashauri ya Kigoma Ujiji.

Wapinzani walitwaa umeya kwenye majiji ya Dar es Salaam, Arusha na Mbeya huku ikiongoza halmashauri za Kinondoni (ambayo imegawanywa), Ilala (Dar es Salaam), Iringa Mjini, Moshi Mjini, Hai, Rombo, Moshi Vijijini na Siha (Kilimanjaro), Tunduma na Mbeya Mjini (Mbeya).

Pia wameshika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Monduli, Karatu, Arumeru Mashariki, Arumeru Magharibi (Arusha), Babati Mjini (Manyara), Manispaa ya Bukoba na mji wa Kayanga (Kagera).

Wapinzani pia wameshika Manispaa ya Tandahimba, Mtwara Mjini na Newala Mjini huku mkoani Lindi ikichukua Kilwa.

Mkoani Mara, Chadema inaongoza Halmashauri ya Serengeti, Tarime Vijijini na Tarime Mjini, wakati mkoani Morogoro Chadema inaongoza Halmashauri ya Mji wa Ifakara.

Awali katika mgogoro huo, Kihamia alitangaza kukata posho za nauli za madiwani wa Arusha kutoka Sh60,000 hadi Sh10,000 na kufuta posho za mafuta ya Sh100,000 kwa mwezi na Sh150,000 za mawasiliano kwa mwezi .

Kitendo hicho kiliwafanya madiwani hao kuitisha kikao na kujadili mkakati wa kupambana na mkuregenzi huyo wakimtaka awape waraka wa kutengua malipo hayo yaliyopitishwa na Serikali mwaka 2008.

Mvutano kuhusu posho pia ulimhusisha mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti aliyetoa agizo kwa wakuregenzi kuacha kuwalipa madiwani Sh40,000 za nauli, badala yake walipwe kwa kufuata bei elekezi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene azungumzie sera ya Serikali kuhusu malipo ya madiwani, alisema kama posho hizo zilikuwa zinakiuka sheria na taratibu, ni “busara kuzifuta”.

Alisema jambo jema ni posho hizo kutumika kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu, hivyo haoni kama kuna jambo limeharibika.

“Ikiwa kuna jambo limevunja sheria, hao wanaolalamika waseme ni sheria zipi. Ninachoona hapo ilitumika busara,” alisema Simbachawene.

“Badala ya kulipana posho huku watendaji wengine wanapata taabu, fedha zimetumika kuwalipa na kuziondoa. Kama wamefuata taratibu, hakuna kilichoharibika.”

Lakini, meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema juzi kuwa mkurugenzi huyo alikata posho bila ya kufuata taratibu na kupinga kitendo cha kufunga shule, akisema nacho hakikufuata taratibu.

“Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inawataka viongozi wote wa umma, na katika muktadha huu wa Jiji la Arusha kufuata miiko na maadili ya uongozi kwa kuwa wanapaswa kuwa wakweli, wawazi na waadilifu,” alisema Meya Lazaro.

Alisema msimamo wa Chadema kuhusu posho ni kuzifuta ili fedha hizo zitumike kuboresha mishahara na stahiki za watumishi wa umma. “Si kweli kwamba madiwani wa Chadema wamejiongezea posho za vikao bali ziliidhinishwa tangu mwaka 2008 wakati halmashauri ikiwa chini ya meya wa CCM, Lawrence Heddi,” alisema.

“Wakati huo mbunge alikuwa Felix Mrema na wajumbe wote wa kamati ya fedha walikuwa CCM na mwenyekiti wake alikuwa Jubilate Kileo (marehemu).”