Lowassa asema wananchi wanajengewa hofu, chuki kuwachagua viongozi wasiowataka

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akichangia mada kuhusu chaguzi na mustakabali wake katika Kongamano la kigoda cha  Mwalimu Nyerere linaloendelea jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Mwenyekiti wa Kongamano, Profesa Rwekaza Mukandala na Katikati ni Katibu Mkuu wa chama cha CCM, Bashiru Ally. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Waziri Mkuu wa zamani Edard Lowassa amesema si kweli kuwa nchi ina viashiria vya uvunjifu wa amani bali wananchi wamejengewa hofu na chuki wawachague watu wasiotaka.


Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani,  Edward Lowassa amesema nchi haina viashiria vya uvunjifu wa amani katika chaguzi za marudio bali wananchi wamejengewa hofu na chuki wawachague watu wasiotaka.

Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 12, 2018  wakati akichangia mjadala katika mdahalo wa kumbukizi ya miaka 19 ya Tanzania bila Mwalimu Julius Nyerere .

“Mzee Butiku (Joseph- mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya Mwalimu Nyerere) amesema jana (katika mdahalo huo) walizungumza juu ya  amani na wakasema kuna viashiria vya kukosekana kwa amani. Mimi neno hilo halinitoshi,  msamiati huo nauhitaji uwe mkali kidogo,” amesema Lowassa.

“Mimi naona nchini kuna hofu na chuki. Inajengwa hofu kubwa kwa wananchi inayowafanya wawachague watu wasiotaka kuwachagua.”

Lowassa ametoa mfano wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa Monduli, akibainisha kuwa  kulikuwa na gari za vyombo vya ulinzi na usalama  45, pamoja na magari ya maji ya kuwasha.

“Kamji kale (Monduli) kakawa kamezungukwa na magari ya jeshi utafikiri kuna vita. Vitu hivyo vinafanywa kwa kutumia vyombo vya dola kusimamia uchaguzi, inakuwa ni taabu sana,” amesema.

Amesema wenzake waliouponda Uchaguzi Mkuu wa Kenya,  binafsi aliupenda kwa sababu waliwafuata watu waliofanya makosa kwenye tume ya uchaguzi kwa kuwapeleka mahakamani na kuadhibiwa.

Amesema nchini inapaswa watizamwe watu hao kwa sababu wanaosimamia uchaguzi Tanzania ni watumishi wa Serikali na wanalipwa na Serikali, hivyo hawawezi kuacha Serikali ianguke.

Amesema miongoni mwa watumishi hao, wapo waliosema waziwazi kuwa hawawezi kuiacha Serikali ianguke, kufafanua kuwa zimewekwa mbinu ili wapinzani wasishinde chaguzi za marudio.

“Kuna chuki mbaya sana  imefikia hatua mwanachama wa Chadema na CCM wanachukiana. Inatia hofu kwa wananchi,” amesema.

Amesema ipo haja ya kuzungumza na wananchi  ili waachane na chuki  na kutokuwa na hofu huku akigusia mapendekezo ya Katiba Mpya yaliyotolewa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.

“Haitoshi kuwaambia kuna viashiria (vya hofu na chuki), waambiwe wazi hili na hili si sawa, ”amesema Lowassa.

Amesisitiza kuwa bila demokrasia hakuna haki na  bila haki hakuna demokrasia.

Alipoanza kuchangia mjadala huo, mbunge huyo wa zamani wa Monduli, alianza kwa kumpongeza Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akisema kuwa ameusikia moto alioanza nao.