MAKALA YA MALOTO: Lowassa wa 2020 hatamfikia wa 2015

Muktasari:

Upepo mkali wa Lowassa uliiumiza CCM, kwa mara ya kwanza katika siasa za Tanzania.


Katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, matarajio kwa CCM ni Rais John Magufuli kutetea kiti chake; nani atabeba turufu ya upinzani?

Lazima ielezwe mapema kwamba Edward Lowassa wa 2020 hatamkaribia hata nusu yule wa 2015.

Lowassa 2015 aligombea Chadema, alikuwa jina kubwa zaidi katika medani za siasa Tanzania.

Mosi, alivyobadili siasa za nchi, ilitoa uthibitisho kuwa Lowassa alikuwa mbabe asiyepimika kwa yeyote.

Pili, akiwa mgombea urais anayewania tiketi ya CCM, chama hicho kilitumia nguvu kubwa kumkata. Hakuna mgombea aliyekiumiza kichwa chama hicho kama Lowassa. Kilitumia muda mrefu kujiandaa kumkata.

Tatu, upepo mkali wa Lowassa uliiumiza CCM. Kwa mara ya kwanza katika siasa za nchi, chama hicho kinatawala huku kikiwa ‘mpangaji’ Dar es Salaam. Dar ndilo jiji ‘bize’ kuliko yote nchini, lakini wapinzani wana madiwani wengi kuliko CCM.

Mwaka 2015, CCM ilipoteza majimbo sita kati ya 10. Ubungo, Kibamba, Kawe, Ukonga, Temeke na Kinondoni yalikwenda Chadema na CUF, huku CCM ikibaki na majimbo manne ya Ilala, Mbagala, Segerea na Kigamboni. Hata hivyo, CCM imerejesha majimbo mawili, Ukonga na Kinondoni kupitia uchaguzi mdogo.

Zaidi, CCM haina cha kujivunia ushindi wa Jimbo la Segerea, kwa kuwa iliupata kama bahati baada ya Ukawa kujichanganya na kusimamisha wagombea wawili; Anatropia Theonest (Chadema) na Julius Mtatiro (CUF) ambao kwa jumla walivuna kura asilimia 58 dhidi ya asilimia 42 alizopata Bona Kalua wa CCM.

Nne, upepo wa Kaskazini ulikuwa mkali kuwahi kutokea. CCM ilipata majimbo mawili tu Kilimanjaro, vivyo hivyo Arusha ambako Ukawa walifanya kufagia pamoja na Manyara.

Hayo ni matokeo ya kishindo cha Lowassa. Na kama angefanya uamuzi wa kuhama CCM mapema, hivyo kujiandaa kwa muda mrefu zaidi, huenda upinzani ungetisha zaidi.

Aliipeleka puta CCM

CCM haitasahau presha kubwa kutoka kwa Lowassa wakati ilipokuwa kwenye mchakato wa ndani wa kumpata mgombea urais.

Kulikuwa na shinikizo la hali ya juu kuonyesha kuwa chama hakina namna zaidi ya kumuidhinisha Lowassa kuwa mgombea urais.

Na kwa picha iliyoonekana dhahiri ni kwamba chama kilikuwa na wakati mgumu zaidi pengine kuliko kipindi chochote kile katika historia tangu kilipoasisiwa. Mwanachama alionekana wazi kukizidi nguvu.

Lowassa alionyesha ufahari wa hali ya juu wakati wa kusaka tiketi ya kugombea urais. Kwa kumlinganisha na wagombea wengine, ilikuwa sawasawa na kuichukua Barcelona iliyokamilika, ije icheze Ligi Kuu Tanzania Bara, halafu utegemee Singida United, Azam, Yanga, Simba, Mtibwa, Mbao kuipa ushindani.

Rejea misafara ya kutafuta wadhamini CCM kati ya Lowassa na ile ya wenzake, utakubaliana na mimi kuwa Real Madrid ililetwa Tanzania ghafla kushindana na Ndanda FC au Stand United.

Hivyo, Lowassa hakupata mpinzani yeyote yule wa kulingana uwezo wake. Na kama si viongozi wa juu kusimamia chama, hakuna ambaye angeweza kushindana naye.

Asambaratisha vigogo

Alipokatwa CCM na kutua Chadema na Ukawa, upepo wa upinzani ulibadilika. Wale waliokuwa wakiitwa wababe wa siasa za upinzani nchini, walionekana ‘mabwana wadogo’, wengine walibadili hadi itikadi kisiasa.

Mosi, kwa muda mrefu aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye alikuwa anaonekana kichwa cha upinzani, huku akiwa ameshajiandaa kisaikolojia kugombea urais kupitia mwavuli wa Ukawa.

Kilichotokea ni Slaa kusema waziwazi kuwa bora CCM ishinde kuliko wapinzani. Itikadi yake ilibadilishwa na Lowassa.

Pili, mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba hakuachwa salama na upepo wa Lowassa, kwani aliamua kwa hiari yake kuachia ngazi. Tatu, aligeuza vyama vya siasa vikubwa kutoka katika sura ya utaasisi na kubaki akitazamwa yeye kama tochi ya upinzani na Nne, alipandisha joto la upinzani na kuwapa wengi ubunge.