Lugola aagiza askari wenye sifa kupandishwa vyeo

Muktasari:

  • Ameagiza mapendekezo hayo yakamilike  ndani ya Julai ili kuwasaidia  askari wenye sifa na ambao wamekaa muda mrefu bila kupandishwa vyeo.

Dar es Salaam.Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu kuandaa mapendekezo ya kuwapandisha vyeo askari wote wenye sifa.

Ameagiza mapendekezo hayo yakamilike  ndani ya Julai ili kuwasaidia  askari wenye sifa na ambao wamekaa muda mrefu bila kupandishwa vyeo.

Lugola  ametoa agizo hilo leo Julai 11 alipotembelea Gereza la Ukonga  na kuzungumza na maofisa na askari wa magereza kutoka vituo mbalimbali vya Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema tayari ameshakula kiapo cha kuwa mwenyekiti wa tume ya magereza na polisi ambayo ina kazi mbalimbali ikiwamo kuwapandisha vyeo askari.

Amesema viongozi wenye chuki binafsi na askari watakaokataa kutoa mapendekezo kwa askari wenye sifa za kupanda vyeo wakati wana sifa hatawavumilia.

“Sitokubaliana na hali hii.  Nataka nidhamu na hali itendeke kwa askari wote wenye sifa za kupanda vyeo. Naomba kwenye mchakato wa mapendekezo kwa askari wenye sifa hali itendeke, atakeyefanya kinyume atakiona cha mtema kuni," amesema Lugola.

 

Lugola ambaye pia mbunge wa Mwibara amewataka askari magereza kufanya kazi kwa bidii na weledi na kukaa mkao wa kula wa kupanda vyeo siku zijazo

Mbali na hilo, Lugola amemuagiza pia katibu mkuu huyo kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa Agosti askari wote wanalipwa mishahara stahiki kulingana na utendaji wao.

"Sitaki kuona askari analipwa mshahara tofauti, wakati anastahili kulipwa kulingana na utendaji kazi wake. Askari ambao mishahara yao haijarekebishwa naomba orodha yao pia," amesema.

Pia, amemtaka Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa kuandaa orodha hiyo na sababu za askari hao kutorekebishiwa mishahara yao ili aweze kulitatua.