Lugola amuagiza DCI amkamate aliyekuwa mkurugenzi Nida

Muktasari:

  • Ameagiza kukamatwa kwa wamiliki wa kampuni tatu zilizohusika na mradi wa vitambulisho vya taifa.

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemuagiza Mkurugenzi wa Makosa Jinai nchini (DCI) kumkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu kabla ya saa 12 jioni leo.

Lugola pia ameagiza kukamatwa kwa wamiliki wa kampuni tatu zinazodaiwa kuhusika katika mradi wa vitambulisho vya taifa, Gotham's International Limited, Gwiholoto Impex Ltd na Aste Insurance wanaodaiwa kufanya udanganyifu na kushindwa kurejesha fedha walizotumia kinyume na utaratibu.

Akizungumza na wanahabari leo Agosti 21, Lugola ameagiza kukamatwa watumishi wote wa Nida ambao wanatuhumiwa katika ubadhirifu wa fedha za umma wakishirikina na kampuni hizo.

“Hizi kampuni zimefanya udanganyifu zikishirikiana na baadhi ya wafanyakazi,”amesema.

Hata hivyo amesema baadhi ya kampuni zilizohusika na ubadhirifu huo zimeanza kurejesha fedha za umma kwa asilimia 84.