Lugola aonya polisi kushirikiana na mafisadi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akiliangalia panga alilopewa na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ikiwa ni kiashiria cha kupewa ushujaa katika jamii ya Kabila la Wagita, baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Kibara, Mkoani Mara, jana. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani

Muktasari:

Amesema mafisadi hao hukimbilia kufungua kesi vituoni wakilazimisha ardhi iwe mali yao na kuwaonya askari wanaoshirikiana nao katika dhuluma hiyo.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema baadhi ya polisi wanashirikiana na mafisadi kudhulumu ardhi ya wananchi maskini.

Amesema mafisadi hao hukimbilia kufungua kesi vituoni wakilazimisha ardhi iwe mali yao na kuwaonya askari wanaoshirikiana nao katika dhuluma hiyo.

Alisema hayo mwishoni mwa wiki akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ragati kata ya Kasuguti, Bunda akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo jimboni mwake.

Waziri Lugola alisema amepata malalamiko mengi kutoka sehemu mbalimbali nchini kuwa mafisadi huonea wananchi maskini kwa kupora ardhi wakidai wao ndio wamiliki. Ili kufanikisha hilo, alisema huwatumia polisi wasiokua waaminifu kuwakandamiza wananchi.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani jana, imemkariri Lugola ambaye ni mbunge wa Mwibara akionya wananchi wasikurupuke kukimbilia kituo cha polisi kufungua kesi za ardhi ambazo hazina uthibitisho wa jinai.

Badala yake, ameagiza kesi au malalamiko yapelekwe katika mabaraza ya ardhi ya eneo husika ili yatatuliwe kwanza.

Alisema mafisadi wanapoona mmiliki halali wa ardhi anagoma kuondoka eneo husika, hutumia fedha kukimbilia polisi kufungua kesi bila uthibitisho na askari wasio waaminifu husaidia kufanikisha mwananchi kunyang’anywa ardhi hiyo.

Alisema endapo kesi ya mlalamikaji yeyote ipo mahakamani anapaswa kuheshimu Mahakama na si kufanya usumbufu katika jamii na kwenda polisi kutafuta njia ya kumsumbua mwananchi.

Lugola alisema endapo mwananchi ana hukumu ya Mahakama inayoonyesha ameshinda kesi, anapaswa kwenda polisi na nakala ya hukumu.

“Rais John Magufuli alianzisha Mahakama ya Mafisadi, kwa taarifa niliyonayo, ina uhaba wa mafisadi, sasa mimi nitaitafutia wateja kwa kuhakikisha wale mafisadi ambao huonea wananchi, hutesa wananchi, huiba fedha za Serikali au taasisi yoyote nitawafikisha katika mahakama hiyo, hatutakubali unyanyasaji wa aina yoyote,” alisema Lugola akiapa kwamba hatacheka na mafisadi, bali atapambana nao na yupo tayari kwa lolote.

Lugola alisema ameanza kupambana na mafisadi ndani ya wizara na tayari wameanza kurudisha fedha za Serikali.

Mwanzoni mwa mwezi huu akizungumza na waandishi wa habari, Lugola alisema kampuni saba zinazodaiwa kufanya ufisadi wa Sh28.5 bilioni katika mradi wa mfumo wa utambuzi uliokuwa ukitekelezwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), zimeanza kurejesha fedha.

Ufisadi huo uligundulika katika ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Februari 2016.

Alisema miongoni mwa kampuni hizo, BMTL imekwishamalizana na Serikali kwa kurejesha Sh569.1 milioni ilizokuwa inatakiwa kulipa.

“BMTL hawa Nida walikuwa wamepanga katika jengo lao la Victoria, lakini kwa muda mrefu walidanganya kuwa eneo ambalo Nida wamelipanga ni mita za mraba 2,201, lakini ikaja kubainika kuwa vipimo ni vya udanganyifu. Ilikuja kubainika eneo lililopangishwa lina ukubwa wa mita za mraba 1947,” alisema.

Lugola alizitaja kampuni nyingine ambazo aliagiza zifike mjini Dodoma na fedha zinazotakiwa kurejesha kwenye mabano kuwa ni Gotham International (Sh2.8 bilioni), Iris Corporation Berhard (Sh22.9 bilioni), Gwiholoto Impex (Sh946.4milioni), Skyes Travel Agent (Sh6 milioni), Dk Shija Paulo Rimoy (Sh27 milioni) na Aste Insurance (Sh 1.2 bilioni).